Na Moses Ng'wat, Tunduma.
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, amesema Wizara yake inatarajia kuanzisha mfumo maalum wa kidijitali utakaowawezesha vijana kufikisha mawazo, ushauri na changamoto zao moja kwa moja serikalini ili hatua zichukuliwe kwa haraka na ufanisi.
Nanauka aliyasema hayo Novemba 25, 2025, mara baada ya kuwasili mkoani Songwe kwa ziara ya kukutana na kuzungumza na vijana kuhusu masuala ya ajira, uwezeshaji kiuchumi na maendeleo ya ustawi wa kundi hilo.
Nanauka akiwa katika mji wa Tunduma alitembelea na kuzungumza na makundi ya vijana katika maeneo ya Sogea Stendi, Kilimanjaro, Kisimani, Stendi ya zamani Majengo na Mpemba.
Akiwa Stendi ya zamani ya Majengo, Waziri Nanauka alisema Wizara imejipanga kuwekeza kwenye TEHAMA kwa kuanzisha mfumo maalum utakawezesha vijana kutoa maoni, pamoja na kurahisisha utolewaji wa majibu ya changamoto zao.
“Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeanzisha Wizara maalum kwa ajili ya vijana ili kusimamia kwa umakini masuala yao na kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa,” alisema.
Hata hivyo, ziara hiyo iligubikwa na malalamiko kutoka kwa vijana wa mji wa Tunduma, waliolalamikia Jeshi la Polisi kwa vitendo vya kuwakamata ovyo bila sababu za msingi, hususan wanapotoa kero mbele ya viongozi wa kitaifa.
Mwenyekiti wa umoja wa bajaji, Hamisi Mwinyi, alisema vijana wamekuwa wakinyanyaswa wanapotekeleza majukumu yao au wanapotoa hoja kwa viongozi.
Akijibu malalamiko hayo, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Jabir Omary Makame, alikiri kuwepo kwa baadhi ya matukio ya ukamataji, akibainisha kuwa baadhi ya vijana wamekuwa wakichukuliwa hatua kwa kuweka urembo na taa zenye mwanga mkali kwenye bajaji—ambazo zinahatarisha usalama barabarani.
Hata hivyo, alisitisha mara moja tozo zinazotozwa na polisi kwenye vituo vya ukaguzi, akizitaja kuwa ni vitendo vya rushwa visivyokubalika.
Waziri Nanauka aliwataka viongozi wa Mkoa wa Songwe na Halmashauri ya Mji wa Tunduma kushughulikia changamoto hizo kwa haraka, akisisitiza kuwa serikali inalenga kuona vijana wakifanya kazi katika mazingira salama na rafiki.
0 Comments