Header Ads Widget

MZUMBE NA REKODI YA UBORA VYUO VYA ELIMU YA JUU

 

NA FARIDA MANGUBE,MATUKIO DAIMA MEDIA MOROGORO

Chuo Kikuu Mzumbe kimeendelea kujiimarisha kama moja ya taasisi bora za elimu ya juu nchini baada ya kutangaza ongezeko kubwa la ubora wa elimu, utafiti na miundombinu, huku kikitoa jumla ya wahitimu 5,901 katika mahafali yake ya 24 katika kamapas zake zote.

Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa William Mwegoha, amesema mafanikio hayo ni uthibitisho wa kazi kubwa iliyofanywa na chuo katika kipindi cha mwaka wa masomo 2024/2025.



Akizungumza wakati wa mahafali hayo, Prof. Mwegoha amesema chuo kimefanikiwa kuongeza uwezo wa usimamizi wa masomo ya Uzamivu (PhD), hatua iliyosaidia kuongeza idadi ya wahitimu wa PhD kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa tangu kuanzishwa kwa chuo kwani mwaka 2023 walikuwa 6 na mwaka 2024 walikuwa 12.


Amesema maboresho ya miundombinu kupitia Mradi wa HEET pamoja na miradi ya ndani, yakiwemo majengo ya taaluma, TEHAMA, mabweni na kituo cha afya, yamechangia kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, huku upanuzi wa barabara, hosteli na jengo la utawala ukiendelea kwa kasi.

Akizungumza katika mahafali hiyo Mkuu wa Chuo na Rais Mastafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein ameongeza kuwa mafanikio haya yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na uwekezaji unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, hususani katika kuimarisha elimu ya juu na utafiti.


Katika wosia wa mahafali, Mlau Prof. Lulu Genda  amewataka wahitimu kuongeza maarifa na kuendeleza utafiti, akisisitiza umuhimu wa fikra huru na kuchambua mambo kwa kina. “Elimu ni bahari  haitulii. Msikubali kubebwa na mawimbi; fikirini, tafuteni na fuatilieni maarifa,” amesema Mlau.

Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Profesa Saida Yahya-Othman, amepongeza wahitimu na kueleza kuwa jitihada za chuo katika kuboresha ubora wa elimu na utafiti zimeanza kuzaa matokeo makubwa.


Katika maafali hiyo Melina Baradyana mwanafunzi wa shahada ya awali ya usimamizi wa mazingira ametambuliwa kuwa Mwanafunzi Bora kwa kuonesha umahiri wa kipekee katika masomo na nidhamu, akielezwa kuwa mfano wa ubora unaoendelezwa na Mzumbe.

MWISHO 


KARIBU TUFUATILIE MATUKIO DAIMA MEDIA NA KARIBU KUTANGAZA NA MATUKIO DAIMA MEDIA KUPITIA INSTAGRAM, TIKTOK, FACEBOOK, X, APP NA CHANEL YA MATUKIO DAIMA TV PIGA SIMU 0754026299


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI