Header Ads Widget

TANZANIA YAANZA UKUSANYAJI MPYA WA TAKWIMU ZA UZALISHAJI WA ASALI

 


Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma

WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeanza mafunzo maalum ya maandalizi ya ukusanyaji takwimu za uzalishaji wa asali, hatua inayolenga kuboresha ubora wa taarifa za sekta ya ufugaji nyuki na kuongeza mchango wake katika uchumi wa taifa.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa TFS, Hussein Msuya, amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa uzalishaji wa asali duniani, na taarifa sahihi za uzalishaji ni msingi muhimu katika kupanga na kuendeleza sekta hiyo.


 “Zamani tulikuwa tunatumia makisio kutoka Shirika la Chakula Duniani (FAO) yaliyofanywa tangu mwaka 2016 walikuwa wanatoa takwimu za chini, za kati au za juu bila uhakika kupitia mafunzo haya, tutaweza kupata takwimu halisi za uzalishaji wa asali, mazao ya nyuki, idadi ya wafugaji, mizinga na hata aina ya mimea inayotumika katika uzalishaji,” amesema Msuya.


Msuya amesisitiza kuwa takwimu hizo zitasaidia kubaini maeneo yenye uzalishaji mkubwa, idadi ya wafugaji na fursa za uwekezaji katika sekta hiyo.

Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu Frida Kundi kutoka makao makuu ya TFS, amesema mafunzo hayo yanahusisha wataalam kutoka kanda saba za TFS nchini, ambao watakwenda kukusanya takwimu katika mikoa mbalimbali.


 “Takwimu hizi ni muhimu kwa nchi na taasisi katika kupanga mipango ya maendeleo, kusaidia jamii na kuongeza mchango wa sekta ya nyuki katika uchumi kwa TFS, taarifa hizi zitatuongoza hata tunapotafuta wataalam wa kuajiri kulingana na mahitaji ya sekta,” amesema Kundi.



Naye Stanislaus Lukiko, mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI), alisema wameungana na TFS kuongeza nguvu ya kitaalamu katika kazi hiyo kwa kuwa changamoto ya takwimu imekuwa ikikwamisha maendeleo ya ufugaji nyuki kwa miaka mingi.


“Suala la takwimu limekuwa changamoto tumekuja kuongeza utaalamu ili kuhakikisha taarifa tutakazokusanya ni sahihi, za uhakika na zinazoweza kutumika katika kupanga maendeleo ya sekta hii muhimu,” amesema Lukiko.



Mafunzo haya yanatarajiwa kutoa mfumo mpya wa ukusanyaji wa takwimu za uzalishaji wa asali nchini, hatua inayotarajiwa kuongeza uwazi, uaminifu na maendeleo ya sekta ya nyuki nchini Tanzania.


Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI