![]() |
| Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Mafunzo ya Lishe kutoka TFNC, Dkt. Esther Nkuba akitoa elimu kwa Wazazi na Walezi (hawapo pichani)shule ya Msingi Mabatini iliyopo Temeke, November 19, 2025 |
Na.Mwandishi Wetu, Temeke.
TAASISI ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) imeendelea kutoa elimu kwa Wazazi na Walezi wa Wanafunzi wa shule za Msingi Manispaa ya Temeke juu ya umuhimu wa Wanafunzi kupata chakula shuleni.
Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Mafunzo ya Lishe kutoka TFNC, Dkt. Esther Nkuba amesema kwa kushirikiana na Manispaa ya Temeke kupitia mradi wa Afya na Lishe unaotekelezwa katika shule za msingi 15 za Manispaa hiyo, kupitia uwezeshaji Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP)
"Tunakutana na Wazazi na walezi wa Wanafunzi na kuwapa elimu sahihi ya umuhimu wa chakula na lishe.
Aidha, amebainisha kuwa, vyakula vinavyouzwa kataka maeneo ya shule mara nyingi haviandaliwi kwa kuzingatia vigezo vya ubora na usalama wa afya, hivyo kuwaweka watoto katika hatari ya kupata magonjwa mbalimbali ikiwemo kisukari, magonjwa ya moyo na baadhi ya saratani kutokana na matumizi makubwa ya mafuta, sukari na chumvi.
“TFNC kupitia mradi huu wa afya na lishe shuleni unaotekelezwa kwa uwezeshaji wa WFP, tumewajengea uwezo pia Walimu wakuu, Walimu wa lishe na wapishi wa shule kuhusu maandalizi sahihi ya chakula, mpangilio wa mlo kamili, usafi na usalama wa chakula ili kuhakikisha wanafunzi wanapata lishe bora,” amesema Dkt. Nkuba.
Dkt Nkuba pia amewataka wazazi na walezi kuendelea kuchangia huduma ya chakula shuleni ili kuhakikisha kila mtoto anapata mlo akiwa shuleni, hatua itakayosaidia kuongeza umakini, kupunguza utoro na hatimaye kuinua ufaulu.
TFNC hadi sasa imeweza kufikia shule mbali mbali za Manispaa ya Temeke, zikiwemo Shule ya Msingi Charambe, Shule ya Msingi Unubini, Shule ya Msingi Mabatini, Shule ya Msingi Ali Hassan Mwinyi na zingine.









0 Comments