Header Ads Widget

MAHAFALI YA MULEBA LUTHERAN VTC,YAFANA MKUU WA CHUO AJIVUNIA USHIRIKIANO.

 

Na Shemsa Mussa -Matukio Daima Media

 Muleba Kagera 

Mahafali ya Chuo cha Muleba Lutheran VTC yamefana kwa kiwango kikubwa, huku Mkuu wa Chuo hicho, Bw. Jaspa Elias Masilingi, akieleza kujivunia mafanikio yaliyopatikana ndani ya miezi mitatu tangu achukue uongozi.

Akizungumza wakati wa mahafali hayo, Bw. Masilingi alisema amefurahishwa na ushirikiano alioupata kutoka kwa wazazi, walimu na wanafunzi, hali iliyompa faraja na kumtia moyo kuendelea kuleta matokeo bora katika taasisi hiyo.

Bw. Masilingi alifafanua kuwa chuo hicho kimesajiliwa chini ya Wizara ya Elimu kwa utoaji wa mafunzo stadi, na kwamba jumla ya wanafunzi 17 wamehitimu baada ya kusoma kwa kipindi cha miaka miwili katika fani za Tehama na Umeme wa Majumbani.

Baadhi ya wahitimu, akiwemo Ashrafu Sadu na Malina Alistides, walisema elimu na ujuzi waliopata chuoni hapo umewaandaa kujitegemea na kuisaidia jamii. Wamekiri kuwa pamoja na kusoma fani kuu mbili, wamepata pia maarifa ya kilimo ikiwemo kulima mbogamboga, matunda na ndizi—ujuzi ambao wamesema utawasaidia kujikimu kimaisha.

Kwa upande wao, wazazi wa wahitimu waliushukuru uongozi wa chuo kwa kuwapatia vijana wao elimu ya ujuzi itakayowawezesha kuajiriwa au kujiajiri katika mazingira ya sasa ya kiuchumi.

Mgeni rasmi, Bw. Luther Lutashobya kutoka ELCT Bukoba, aliwataka wahitimu wa Tehama kuitumia vyema fursa ya ukuaji wa teknolojia, akibainisha kuwa dunia sasa inategemea mtandao, hivyo ujuzi wao unahitajika zaidi. Aliwatia moyo kuendelea kujifunza, kuwa waaminifu na kuzingatia maadili ili wapate kuaminika na kufungua milango ya fursa zaidi.

Bw. Lutashobya alikemea tabia za baadhi ya watu wenye vyeo ambao hawatimizi wajibu wao ipasavyo, akisisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii na uadilifu.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI