Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Emmanuel John Nchimbi ameshiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) ukiwa ni mkutano wake wa kwanza kushiriki nje ya mipaka ya Tanzania kumwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,
tangu alipoapishwa kushika wadhifa huo Novemba 03, 2025.
Mkutano huo uliofanyika Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Novemba 15, 2025 umefunguliwa na Rais wa DRC, Mhe. Felix Tshisekedi ambaye alipokea uenyekiti wa Jumuiya hiyo kutoka kwa Rais wa Angola, Mhe. João Lourenço.
Katika hotuba yake ya ufunguzi Rais Tshisekedi alimpongeza Rais Samia kwa ushindi na kuendesha uchaguzi ulio huru, haki na wazi uliofanyika Oktoba 29, 2025.
Aidha, Rais Tshisekedi pamoja na viongozi wengine waliopata fursa ya kuhutubia mkutano huo wakiwemo Katibu Mtendaji wa ICGLR, Balozi João Samuel CAHOLO, Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Afrika, Mhe. Mahamoud Ali Youssouf na Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe. António Guterres walisisitiza umuhimu wa chombo hicho kuendelea na jukumu la kuimarisha amani, usalama na maendeleo katika nchi wanachama.
Walitoa wito kwa nchi wanachama zirejee katika misingi ya uanzishwaji wa Jumuiya hiyo kwa kuiwezesha rasilimali ili ICGLR iweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
ICGLR iliyoanzishwa mwaka 2006 kwa lengo la kuleta amani, usalama na maendeleo katika nchi wanachama itasherehekea maadhimisho ya miaka 20 mwaka 2026 na inatarajiwa katika maadhimisho hayo nchi wanachama zitafanya tathimini ya utekelezaji wa malengo yake.










0 Comments