Na OWM - TAMISEMI, Karatu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amesema Serikali kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) itajenga barabara ya kijiji cha Mang’ola Barazani yenye urefu wa Kilomita 10.8 iliyopo wilayani Karatu, ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa wananchi wa kijiji hicho kinachozalisha vitunguu vyenye thamani ya Bilioni 1.2 kwa mwaka.
Prof. Shemdoe ametoa aahadi hiyo ya Serikali Machi 06, 2026 kwa wananchi wa kijiji hicho, alipopewa fursa na Mhe. Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba ya kuwasalimia wananchi hao, mara baada ya Mhe. Waziri Mkuu kuweka Jiwe la Msingi la Mradi wa Ujenzi wa Skimu za Umwagiliaji katika Bonde la Eyasi na kupokea kero ya ubovu wa barabara hiyo ya Mang’ola Barazani.
“Kijiji cha Mang’ola kwa mwaka kinazalisha vitunguu vyenye thamani ya Bilioni 1.2, kimsingi miundombinu ya barabara ya Mang’ola Barazani inatakiwa kuboreshwa kutokana na umuhimu wake na itaboreshwa mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa barabara za Kilomita 15 za Karatu Mjini,” amesisitiza Prof. Shemdoe.
Akizungumzia hatua ya awali iliyochukuliwa na ofisi yake, Prof. Shemdoe amesema katika Mwaka wa Fedha 2025/26 kiasi cha Shilingi Milioni 73 kimetengwa na TARURA ili kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha changarawe ambayo ina urefu wa Kilomita 10.8.
Prof. Shemdoe ameanisha kuwa, barabara hiyo ikijengwa itatumiwa na wananchi kwa shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi, ikiwemo usafirishaji wa mazao ya kilimo kama vitunguu, mpunga na mahindi kwenda kwenye masoko na kuongeza kuwa, itawawezesha wananchi kufikia huduma za jamii zikiwepo za afya na usafiri wa kila siku kwa kutumia magari madogo na pikipiki.
Barabara ya Mang’ola Barazani inayopita katika Bonde la Ziwa Eyasi ni mojawapo ya miundombinu muhimu inayowaunganisha wananchi wa Kata ya Mang’ola na maeneo ya jirani pamoja na mji wa Karatu mkoani Arusha, na maboresho yake yanatarajiwa kuongeza tija ya uzalishaji na biashara ya mazao katika eneo hilo.









0 Comments