*_Atoa rai kwa wananchi kuendelea na shughuli zao za kiuchumi_*
*_Awahakikishia wananchi Ulinzi na usalama wa kutosha_*
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla amewahakikishia wananchi wa Mkoa wa Arusha, wageni na Watalii wanaofika Mkoani Arusha kuwa hali ya ulinzi na usalama Mkoani Arusha ni shwari na shughuli za kijamii na kiuchumi zimerejea katika hali yake ya kawaida.
Mhe. Makalla amebainisha hayo leo Jumanne Novemba 04, 2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake, mara baada ya Kikao cha Kamati ya Ulinzi na usalama ya Mkoa, akisema kwamba Vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga pia kuhakikisha huduma za ulinzi na usalama zinakuwepo muda wote ili kuruhusu shughuli za kijamii na kiuchumi za kila siku kuendelea kama ilivyo kawaida.
Aidha katika kutekeleza maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa hapo jana, CPA Makalla amewataka wamiliki wa Vituo vya mafuta kufungua vituo vyao pamoja na maeneo mengine ya biashara, akiwataka Viongozi wa serikali za Mitaa na Vijiji kuendelea kutimiza jukumu lao la kuhakikisha usalama unakuwepo wa kutosha katika maeneo yao na kutoa taarifa za uvunjifu wa sheria kwa Mamlaka husika.
Katika hatua nyingine CPA Makalla amewaagiza Wakurugenzi watendaji wa Halmashauri zote Mkoani Arusha chini ya usimamizi wa Katibu Tawala wa Mkoa, kuhakikisha huduma za usafi wa mazingira zinasimamiwa kikamilifu kwa kuondoa taka zote kwenye maeneo ya masoko na makazi ya wananchi ili kuepukana na magonjwa ya milipuko kutokana na mrundikano wa takataka.








0 Comments