Header Ads Widget

WAZEE WAASWA KUHAMASISHA VIJANA KUJITOKEZA KUPIGA KURA

 

Na Hamida Ramadhan, MatukioDaima Media Dodoma

WAZEE wametajwa kuwa na nafasi muhimu katika kuhakikisha vijana wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa kidemokrasia kwa kujitokeza kupiga kura. Katika kuelekea uchaguzi wa Oktoba 29, 2025, wazee wa Mkoa wa Dodoma wamehimizwa kutumia busara, hekima na heshima walizonazo kushawishi vijana kujiandikisha na kushiriki kikamilifu katika kupiga kura kwa amani na utulivu.

Akizungumza na wazee wa Mkoa huo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, amesema kuwa vijana ndio nguvu kazi ya taifa na ndiyo msingi wa mabadiliko ya kisiasa, kijamii na kiuchumi, lakini mara nyingi hushindwa kushiriki ipasavyo katika uchaguzi. 

Amesema ni jukumu la wazee, kama nguzo ya jamii, kuwahamasisha vijana kuelewa kuwa kura yao ni sauti ya mabadiliko.


"Ninyi wazee mmekuwa mashahidi wa historia ya nchi hii. Mnao uwezo mkubwa wa kuwashauri vijana kuhusu umuhimu wa kushiriki katika maamuzi ya nchi kupitia sanduku la kura. Msiwaache wajisikie hawana nafasi  waambieni kura ni haki yao na wajibu wao," amesema Mhe. Senyamule.


Aidha, amesisitiza kuwa malezi ya kizazi kijacho hayaishii nyumbani pekee, bali yanajumuisha kuwaongoza vijana kuelekea kwenye misingi ya uzalendo, uwajibikaji na ushiriki wa haki katika masuala ya kitaifa kama uchaguzi.


Kwa upande wao, baadhi ya wazee walionesha utayari wa kushirikiana na Serikali na taasisi nyinginezo kuhamasisha vijana kwa njia mbalimbali ikiwemo mikutano ya kijamii, nyumba za ibada na vikao vya kijadi.


Wazee pia waliombwa kuwahimiza vijana kutunza amani, kuheshimu sheria na kuepuka kuchochewa na maneno ya uchochezi hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi. Ushiriki wa vijana katika uchaguzi sio tu kwa kupiga kura, bali pia kwa kuwa mabalozi wa amani na utulivu katika jamii.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI