"Nimechagua kupanda miti ili kutimiza wajibu wangu kama Mtanzania na kama binadamu ninayewajibika kuitunza na kuhifadhi sayari yetu ya dunia tuliyokabidhiwa na Mwenyezi Mungu lakini vile vile kuacha urithi kwa vizazi vinavyokuja" , Kauli hiyo imetolewa leo Januari 27, 2026 na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipokuwa akishiriki zoezi mama la upandaji miti aliloliasisi mwenyewe katika eneo la Bungi Kilimo, Mkoa wa Kusini Unguja.
Zoezi hilo amelifanya ikiwa ni kumbukizi yake ya siku ya kuzaliwa ikiwa ni ishara mjarabu ya kuirithisha jamii mazingira bora na salama kwa mustakabali wa Taifa la Tanzania na Dunia kwa ujumla.
TANAPA kama kinara wa Uhifadhi Endelevu nchini, kupitia Ofisi Kiunganishi Zanzibar chini ya uongozi wa Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Dkt. Halima Kiwango pia wameshiriki zoezi hilo ili kuunga mkono juhudi za Rais wetu na kuifanya Tanzania kuwa na ikolojia rafiki kwa maisha ya viumbe hai, aidha, katika zoezi hilo zaidi ya miti 1500 ikipandwa ikijumuisha miti ya matunda na miti mingine ya kawaida.
Zoezi hili la upandaji miti pia limeendelea katika Hifadhi ya Taifa Saadani na Ofisi Kiunganishi Dar es Salaam ambapo kwa Hifadhi ya Saadan takribani miti 500 imepandwa.
Kwa upande wa Dar es Salaam zoezi hilo liliendelea likimuhusisha Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Neema Mollel, Mkuu wa ofisi hiyo akiambatana na timu ya maafisa na askari kutoka TANAPA, huku pia likitamalaki katika Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro na kijiji cha Ikanutwa kilichopo wilayani Mbarali mkoa wa Mbeya likihusisha Hifadhi ya Taifa Ruaha.
Katika wilaya ya Mbarali zoezi hilo liliongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Brigedia Jenerali Maulid Sulumbu.









0 Comments