Na mwandishi wetu
Mgombea wa Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameahidi kuwapatia wajasiriamali mikopo isiyo na riba na bila urasimu, ili kuhakikisha fursa za kifedha zinawafikia hadi ngazi za chini zaidi za wajasiriamali visiwani humo.
Dkt. Mwinyi amesema Serikali ijayo chini ya uongozi wake itatenga fungu kubwa la fedha kwa ajili ya mikopo hiyo, lengo likiwa ni kuwawezesha wajasiriamali wengi zaidi kunufaika bila kubebeshwa mzigo wa riba na taratibu ngumu zisizo za lazima.
Ameeleza kuwa Serikali itahakikisha inawaondolea wajasiriamali vikwazo vinavyosababishwa na urasimu, ikiwemo utaratibu wa kusajili vikundi, ambao kwa muda mrefu umekuwa ukikwamisha wajasiriamali wadogo kupata mikopo.
“Tunataka kila kijana, mama lishe, mvuvi, mkulima na mfanyabiashara mdogo awe na nafasi ya kukopa kwa urahisi, bila riba na bila mizigo ya urasimu. Serikali itawafuata kule walipo,” amesema Dkt. Mwinyi.
Aidha, amebainisha kuwa Serikali imeandaa mkakati madhubuti wa kuwafikia wajasiriamali, kuwapatia mafunzo, kuwawekea mazingira bora ya kufanyia kazi na kuhakikisha wanafanya biashara katika mazingira rafiki na yenye tija.
Dkt. Mwinyi amesisitiza kuwa akirejea madarakani katika awamu ya pili, atawaelekeza watendaji wake kushirikiana moja kwa moja na wajasiriamali ili kupata maoni na ushauri wa nini kifanyike katika kuboresha sera na mikakati ya kukuza uchumi wa Zanzibar kupitia sekta hiyo.
Mkutano huo umefanyika katika Ukumbi wa Idrissa Abdulwakil, Kikwajuni, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, na ulihudhuriwa na makundi mbalimbali ya wajasiriamali, wavuvi, wakulima na wadau wengine wa maendeleo, ikiwa ni muendelezo wa kampeni zake za urais.
0 Comments