Header Ads Widget

WANANCHI WA IYAGABUYAGA-BUSEGA WAASWA KUFUATA SHERIA ZA UHIFADHI WANYAMAPORI


 Na Mwandishi Wetu, Simiyu

Serikali imewaasa wananchi wa Kijiji cha Iyagabuyaga, Wilaya ya Busega mkoani Simiyu kufuata sheria, kanuni na taratibu za uhifadhi wa wanyamapori ili kuepuka migogoro na Serikali pamoja na kuendeleza shughuli za uhifadhi endelevu nchini. 

 Afisa Wanyamapori Mkuu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Nassoro Wawa ameyasema hayo Oktoba 6, 2025 katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo kwa lengo la kutoa elimu ya uhifadhi na namna ya kukabiliana na changamoto za wanyamapori wakali na waharibifu, kufuatia tatizo la fisi lililokithiri katika eneo hilo.


Katika utoaji elimu hiyo unaofanywa na Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, TAWA, na Maafisa Wanyamapori wa Halmashauri mkoani humo, Afisa huyo amesema Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori,  inasema kuwa mnyama ni nyara ya Serikali, na ukikamatwa huna kibali ni kosa la uhujumu uchumi."

Amesema Serikali imeweka mazingira rafiki kwa wananchi kushiriki katika shughuli za uhifadhi kisheria, ikiwemo kuanzisha bucha za wanyamapori, bustani, mashamba na ranchi za wanyamapori, hatua inayolenga kuchochea maendeleo na kuongeza kipato kwa wananchi.

“Sheria hizi zimekuja kumuwezesha mwananchi kunufaika na rasilimali za wanyamapori nchini ambazo ziruhusu mwananchi,  kikundi, kijiji kuanzisha bucha ya nyamapori, bustani, shamba na ranchi za wanyamapori ili kuinua kipato na kuleta maendeleo tunayoyataka,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Afisa Uhifadhi kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA),  Lusato Masinde, amebainisha kuwa wananchi wanaruhusiwa kumuua mnyamapori anapothibitishwa kuwa tishio kwa maisha au mali, lakini kwa sharti la kutoa taarifa mara moja kwa viongozi wa Serikali.


“Kama mnyamapori atahatarisha maisha au mali zako, unaweza kumuua lakini lazima utoe taarifa kwa Mwenyekiti wa Kijiji, Mtendaji au Maafisa Wanyamapori. Nyara hizo ni mali ya Serikali na lazima zikabidhiwe sehemu husika,” ameeleza  Masinde.

Aidha, ameonya kuwa mtu yeyote atakayemuua mnyamapori bila kutoa taarifa kwa mamlaka husika atakuwa ametenda kosa na kufuatana na sheria atachukuliwa hatua kali za kisheria, ikiwemo kufunguliwa mashitaka ya uhujumu uchumi na akithibitika atahukumiwa kifungo.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Mwenyekiti wa Kijiji cha Iyagabuyaga, Bw. Bahati Masaga, amesema changamoto ya fisi imekuwa kubwa kijijini hapo, na Serikali ilifanikiwa kuwaua fisi 17 hivi karibuni.

Ameishukuru Serikali kwa kutoa elimu ya kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu na kuahidi wananchi kuendelea kushirikiana na mamlaka husika katika kutatua tatizo hilo na kuwaomba waachane na imani potofu za kishirikina za kufuga fisi. 



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI