Header Ads Widget

WANANCHI WA DODOMA WAASWA KUJITOKEZA KUPIGA KURA, HALI YA USALAMA NI SHWARI


 

NA MATUKIO DAIMA MEDIA.

DODOMA.Ikiwa leo ni Oktoba 29, 2025, siku ya Uchaguzi Mkuu nchini Tanzania, Wananchi wa Mkoa wa Dodoma wenye sifa na waliojiandikisha kwenye Daftari la mpiga kura, wameaswa kujitokeza kwa wingi kwenye vituo vya kupigia kura ili kutimiza haki yao ya Kikatiba kwa kuchagua Viongozi wanaowataka kwani hali ya usalama ni shwari.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ametoa wito kwa wananchi hao alipokua kwenye Kituo alichojiandikishia kupiga kura cha Shule ya msingi Dodoma Mlimani Jijini Dodoma mapema asubuhi ya leo, alipofika kwa lengo la kutimiza haki yake ya Kikatiba.

“Mimi nimetoka nyumbani kwangu mpaka nimefika hapa, sijaona mtu yeyote njiani ambaye anayeonekana kukosa amani, watu wote nimekuta wakiwa na furaha, wanaendelea na shughuli zao, hakuna tishio lolote, Dodoma ipo salama. Wito kwa wananchi wa Dodoma ni wajitokeze kupiga kura wakati ndio huu, siku ndio leo hakuna hofu yeyote ya usalama.”

Sambamba nae, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Dkt. Frederick Sagamiko, ni miongoni mwa watu waliojitokeza mapema kutimiza haki yake katika Kituo hicho ambapo ameipongeza Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi  (INEC) kwa kufanya zoezi kuwa jepesi kutokana na watendaji wake kuwa na weledi, vituo vya kupigia kura kuwa vingi hali inayoepusha foleni.

Aidha ametoa wito kwa wananchi ambao wanasubiri baadae ndipo wajitokeze kwenye Vituo, wajitokeze kwani zoezi la uchaguzi limeanza, wakati ni sasa na wakumbuke kuwa zoezi linatarajiwa kukamilika saa 10:00 jioni hivyo wanapozidi kuchelewa wanaweza kusababisha foleni zisizo na msingi.

Baadhi ya wananchi waliojitokeza kwenye kituo hicho kupiga kura, wamepongeza zoezi hilo kwa kuwa la muda mfupi linalowezesha mtu kuendelea na shughuli nyingine za kiuchumi hivyo, wametoa hamasa kwa wengine ambao bado hawajatoka, wajongee kwenye vituo vyao kupiga kura kwani ni haki yao ya msingi.

Uchaguzi Mkuu unafanyika leo nchini Tanzania ikiwa ni utaratibu wa kila baada ya miaka mitano,kwa lengo la kuwachagua  Rais, Wabunge  na Madiwani. Hiyo ni haki ya Kikatiba ya kila Mtanzania kushiriki katika mchakato huo.

MWISHO.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI