Header Ads Widget

WANAFUNZI MILIONI 1.5 KUFANYA UPIMAJI WA KITAIFA WA DARASA LA NNE KESHO

 

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Dkt. Said Ally Mohamed, amesema jumla ya wanafunzi 1,582,140 wa darasa la nne kutoka shule 20,517 za Tanzania Bara wanatarajia kufanya mtihani wa upimaji wa kitaifa kesho na keshokutwa, Oktoba 22 na 23, 2025.


Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Dkt. Mohamed amesema mtihani huo utafanyika kwa mara ya kwanza katika masomo sita ya msingi ambayo ni Sayansi, Hisabati, Jiografia na Mazingira, Sanaa na Michezo, Kiswahili, English Language, pamoja na Historia ya Tanzania na Maadili.


Aidha, amebainisha kuwa kutakuwa na masomo ya chaguo matatu ambayo ni Kifaransa, Kiarabu na Kichina, ambapo kila mwanafunzi atatakiwa kuchagua somo moja pekee.


Ameeleza kuwa mwongozo huo unatekelezwa kwa mujibu wa Sera ya Elimu ya Mwaka 2014 (Toleo la 2023) na Mtaala ulioboreshwa, unaolenga kuinua ubora wa elimu ya msingi nchini.


Kati ya wanafunzi watakaofanya upimaji huo, wavulana ni 764,290 sawa na asilimia 48.31, huku wasichana wakiwa 817,850 sawa na asilimia 51.69.


Dkt. Mohamed ametoa wito kwa wasimamizi wote watakaosimamia upimaji huo kufanya kazi kwa umakini, uadilifu na kuhakikisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu wanapewa haki zao ipasavyo.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI