Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeanza maandalizi ya kushiriki katika mkutano wa 30 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi COP30 unaotarajiwa kufanyika kuanzia Novemba 10 hadi 21 mwaka 2025 katika jiji la Belém nchini Brazil
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Cyprian Luhemeja amesema hayo jijini Dodoma wakati wa kufungua kikao cha kitaifa cha kupitia na kujadili vipaumbele vya nchi kabla ya kushiriki katika mkutano huo muhimu wa kimataifa
Amesema kuwa kabla ya mkutano huo mkubwa kutakuwa na vikao vya maandalizi kuanzia Novemba 4 hadi 9 mwaka 2025 ambavyo vitajumuisha mkutano wa wakuu wa nchi na serikali unaotarajiwa kufanyika Novemba 6 na 7 katika jiji hilo hilo la Belém
"Mkutano wa mwaka huu ni wa kihistoria kwa kuwa utafanyika katika Brazil ambayo ni miongoni mwa nchi zilizoanzisha mkataba wa mabadiliko ya tabianchi hivyo ajenda zitakazojadiliwa zinatarajiwa kuwa za kina na kuelekeza dunia katika kuchukua hatua madhubuti za haraka kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi baada ya miaka 33 ya mkataba huo kuwepo, " Amesema Luhemeja
Luhemeja amewataka wadau na washiriki wa kikao cha maandalizi kuhakikisha wanajadili kwa kina na kutoa mapendekezo yenye tija ambayo yataisaidia nchi kunufaika zaidi na mkutano wa COP30 hususan katika kupata fursa za kiuchumi kijamii na kimazingira zitakazochangia katika kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi nchini
0 Comments