Header Ads Widget

WAFUGAJI WAASWA KUJITOKEZA KUPIGA KURA OKTOBA 29.

 

NA CHAUSIKU SAID 

MATUKIO DAIMA MWANZA.

Wafugaji kote nchini wamehimizwa kujitokeza kwa wingi kushiriki zoezi la upigaji kura Oktoba 29 mwaka huu, katika uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, ili kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha sekta ya mifugo nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Tanzania, Mrida Mshota, alisema serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya mifugo ndani ya kipindi cha miaka minne.

“Nimefika hapa kuwahabarisha wafugaji wote nchini kujitokeza kupiga kura kwa sababu serikali imetufanyia kazi kubwa. Bajeti ya wizara ya mifugo imeongezeka kutoka shilingi bilioni 169 mwaka 2021 hadi kufikia bilioni 475 mwaka huu,” alisema Mshota.

Mshota ameeleza kuwa serikali  imetenga shilingi bilioni 210 kwa ajili ya kuhakikisha mifugo yote nchini inachanjwa, hatua itakayowezesha Tanzania kuuza mifugo katika masoko makubwa ya kimataifa.

“Tayari shilingi bilioni 69 zimetolewa na kazi inaendelea. Hii ni hatua kubwa kwa wafugaji wetu,” alisema Mshota.

Mshota amesema kuwa chama hicho cha wafugaji kina wanachama zaidi ya 400,268, na anaamini wengi wao watajitokeza kupiga kura ili kuhakikisha maendeleo yaliyopatikana yanaendelezwa.

Aidha, alitaja hatua mbalimbali zilizochukuliwa na serikali, ikiwemo kutatua migogoro kati ya wafugaji na wakulima pamoja na kuondoa migogoro ya ardhi kwenye maeneo ya hifadhi, kuwa ni ushahidi wa dhamira njema ya serikali kwa wafugaji.

“Tulikuwa na migogoro mingi baina ya wafugaji, wakulima na wahifadhi, lakini sasa migogoro hiyo imepungua kwa kiasi kikubwa. Wafugaji wanakopesheka, na hadi sasa zaidi ya wafugaji 8,313 wamepata mikopo yenye riba nafuu yenye thamani ya shilingi bilioni 106.9,” alisema Mashota.

Kwa mujibu wa Mshota, Rais Samia ameahidi kutenga hekta milioni 6 kwa ajili ya wafugaji, sambamba na kuhakikisha upatikanaji wa maji, chanjo, na ardhi ya kufugia katika maeneo mbalimbali nchini.

MWISHO.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI