Na Fadhili Abdallah,Kigoma
AHADI ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoitoa mwaka 2022 ya ujenzi wa soko la Kisasa katika bandari ndogo ya kibirizi mjini imeanza kutekelezwa kufuatia Mamlaka ya Bandari nchini TPA kumkabidhi eneo la ujenzi makandarasi wa Mradi huo.
Mkurugenzi wa huduma za uhandisi TPA,Erick Madinda alisema hayo wakati mamlaka hiyo ikizindua ujenzi wa mradi huo na kumkabidhi Mkandarasi wa mradi huo Kampuni ya KGG Investiment Ltd eneo la ujenzi ili mradi huo uanze kutekelezwa.
Mhandisi Madinda alisema kuwa kiasi cha shilingi Bilioni 6.4 kimetolewa na serikali kwa ajiili ya utekelezaji wa mradi huo ambapo pamoja na soko pia kitajengwa kituo cha polisi huku mradi huo ukitarajia kutumia miezi 12 katika utekelezaji wake.
Mkurugenzi wa huduma za uhandisi Mamlaka ya usimamizi wa bandari nchini (TPA),Erick Madinda (kulia) akitoa maelezo kwa Mkuu wa wilaya Kigoma Rashid Chuacha (wa tatu) Kigoma kuhusu mradi wa ujenzi wa soko na kituo cha polisi katika bandari ndogo ya Kibirizi Manispaa ya Kigoma Ujiji mradi wenye thamani ya shilingi Bilioni 6.4 ikiwa ni utekeleza ji wa ahadi ya Raisi Samia aliyoitoa mwaka 2022 alipofanya ziara mkoani Kigoma.
Akitoa maelezo wakati wa hafla hiyo Meneja wa bandari za ziwa Tanganyika,Edward Mabula alisema kuwa utekelezaji wa mradi huo unafuatia ahadi aliyotoa Rais Samia Suluhu Hassan alipofanya ziara mkoani Kigoma mwaka 2022 ambapo pia alitembelea bandari hiyo na kukuta changamoto ya eneo la awali lililojengwa soko likiwa limezizingirwa na maji kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.
Mabula alisema kuwa katika utekelezaji wa mradi huo kutakuwa na maduka na huduma mbalimbali lakini pia kutakuwa na vibanda 250, vizimba 250,ofisi, migahawa na maeneo ya vyoo ambavyo vitatumiwa na wafanyabiashara lakini pia kutajengwa kituo cha polisi katika eneo hilo.
Akizungumza katika makabidhiano hayo Mkuu wa mkoa Kigoma,Balozi Simon Sirro alisema kuwa ujenzi wa soko hilo katika bandari hiyo ndogo ya Kibirizi utachochea biashara baina ya mkoa Kigoma na Nchi za ukanda wa maziwa makuu, ambazo ni Zambia, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ambapo wasafiri wengi wanatumia bandari hiyo kwenda katika nchi hizo.
Katika hotuba iliyotolewa kwa niaba yake na Mkuu wa wilaya Kigoma,Dk.Rashid Chuachua alisema kuwa alisema kuwa serikali imeuchagua mkoa Kigoma kuwa mkoa kimkakati kiuchumi na biashara hivyo utekelezaji wa mradi huo utachochea katika utekelezaji wa mpango huo kwa soko la nchii za ukanda wa maziwa makuu.
Mwisho.








0 Comments