Chuo cha ufundi stadi VETA kwa kushirikiana na waajiri na wamiliki wa viwanda nchini wamepanga kufanya mkutano wa pamoja wenye lengo la kuboresha mitaala ya VETA.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi (VETA) Antony Kasole katika chuo cha ufundi stadi VETA Mbeya baada ya kutembelea chuo hicho mkoani Mbeya.
Kiongozi huyo mkuu wa VETA, amesema wamedhamiria kufanya mkutano huo kwa lengo la kushauriana ili kuboresha mitaala ya VETA itakayosaidia kuendana na soko la ajira.
Pamoja na hayo ametembelea chuo cha ufundi stadi VETA na kukagua karakana nne zinazotumika kutengeneza bidhaa mbalimbali na baadaye kutembelea banda la Veta kwenye maadhimisho ya wiki ya vijana kitaifa jijini Mbeya.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha ufundi stadi VETA mkoa Mbeya Hassan Kalima akizungumza chuoni hapo, amesema chuo cha VETA Mbeya kinaendelea kuhamasisha jamii kujiunga na chuo hicho ili kutoa mafunzo mbalimbali ambayo ni ya faida kwao na Taifa kwa ujumla.
Nao baadhi ya wanufaika wa chuo cha ufundi stadi VETA wameeleza manufaa ambayo wameyapata kuwa ni pamoja na kupata ujuzi uliowafanya kutotegemea kuajiriwa pekee bali hata kujiajiri.
Pia wamesema kupitia elimu mbalimbali walizojifunza Veta na kujiajiri nao wamefanikiwa kuajiri watu wengine ikiwemo kwenye ufumaji wa nguo na ufundi umeme hivyo kuwasaidia katika kuendesha maisha yao.
0 Comments