Na Shemsa Mussa -Matukio Daima Muleba, Kagera
VIONGOZI wa dini wametakiwa kutumia nafasi zao kuhubiri amani na utulivu hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, ili taifa liendelee kujivunia mshikamano na umoja uliopo.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Bw. Abel Nyamahanga, alipokutana na wazee pamoja na viongozi wa dini katika ikulu ndogo ya wilaya hiyo.
Bw. Nyamahanga amesema ni jukumu la kila kiongozi wa dini kuhakikisha anatumia na nafasi aliyonayo kuhimiza amani, upendo na mshikamano miongoni mwa wananchi bila kujali tofauti za kisiasa, dini au makabila. Amebainisha kuwa viongozi wa dini wana ushawishi mkubwa katika jamii, hivyo maneno yao yanaweza kujenga au kubomoa umoja wa kitaifa.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya amesisitiza umuhimu wa wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwa amani, huku wakiheshimu sheria na taratibu zilizowekwa na Tume ya Uchaguzi. Amesema uchaguzi ni sehemu ya demokrasia, na ni fursa kwa kila mwananchi kuchagua viongozi wanaowaamini kwa mujibu wa Katiba.
“Uhai na usalama wa taifa letu upo mikononi mwa kila mwananchi, hivyo ni jukumu letu sote kuhakikisha tunalinda amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi,” amesema Bw. Nyamahanga.
Pamoja na hayo, amekumbusha wananchi kuwa na utamaduni wa kuwawajibisha viongozi wanaowachagua kwa kuwauliza maswali juu ya utendaji wao, badala ya kulalamika bila kuchukua hatua Amesema uwajibikaji na ufuatiliaji ni nguzo muhimu katika kuimarisha maendeleo ya taifa.
Viongozi wa dini walioshiriki kikao hicho waliahidi kushirikiana na serikali katika kuhamasisha amani na utulivu, huku wakiahidi kutumia nyumba za ibada kama majukwaa ya kuelimisha waumini kuhusu umuhimu wa kushiriki uchaguzi kwa amani na kuheshimu matokeo yatakayopatikana.






0 Comments