Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.
MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Bariadi Mjini kupitia CCM, Mhandisi Kundo Andrea Mathew, ameendelea na kampeni zake zenye kasi na mvuto wa kipekee huku akipiga hatua mtaa kwa mtaa, mguu kwa mguu, kuhakikisha kila mwananchi wa Bariadi Mjini anaelewa dhamira njema na kazi kubwa iliyofanywa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya Watanzania.
Akiwa katika Mtaa wa Nyasosi, Kata ya Somanda, Mhandisi Kundo amekutana na vijana wengi wenye ari na hamasa, na kuzungumza nao kwa ukaribu kuhusu mafanikio makubwa ya Utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyotekelezwa chini ya uongozi wa Dkt. Samia ikiwemo ujenzi wa miundombinu, upatikanaji wa maji safi na salama, Elimu bora, na fursa za ajira kwa vijana.
Katika mazungumzo hayo yenye msisimko, Mhandisi Kundo amewakumbusha vijana kwamba maendeleo hayo hayaji kwa maneno, bali kwa vitendo na ushiriki wa wananchi kupitia kura zao.
Amewahimiza vijana wote wa Mtaa wa Nyasosi na Bariadi Mjini kwa ujumla kujitokeza kwa wingi tarehe 29 Oktoba 2025, siku ya kupiga kura, kuhakikisha wanampigia kura za kutosha Mgombea Urais Dkt. Samia Suluhu Hassan na wagombea wote wa CCM ili kazi ya kuwaletea Maendeleo iendelee na mafanikio yazidi kushamiri.
“Kura yenu ni sauti ya maendeleo...Tukishirikiana na Rais Dkt. Samia, tutaleta Bariadi mpya yenye elimu bora, maji, na miundombinu imara kwa vizazi vyetu.” amesema Mhandisi Kundo.
Ziara hii imeacha hisia kubwa za matumaini na mshikamano kwa vijana wa Nyasosi, ambao wameahidi kujitokeza kwa wingi kuhakikisha ushindi wa kishindo kwa Dkt. Samia na Mhandisi Kundo Oktoba 29, 2025.
Mwisho.












0 Comments