Na Mwandishi wetu.... Matukio Daima.
MWADHAMA Protase Kardinali Rugambwa, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Tabora nchini Tanzania amesisitiza umuhimu wa Jamii kuombwa amani ya Tanzania na mshikamano Miongoni mwa watanzania kama ambavyo Vitabu vitakatifu vilivyoagiza kukaa pamoja kwa umoja.
Kardinali Rugambwa amebainisha hayo leo Oktoba 24, 2025 wakati wa Kongamano la maombi lililofanyika Tabora na kukusisha waumini wa dini na madhehebu mbalimbali Mkoani humo wakati huu wa kuelekea kwenye uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
"Sisi ni watoto wa baba mmoja, tukae pamoja na kuwa tayari kufanya mambo pamoja ikiwemo amani, haki, upendo, ushirikiano, kwamba umoja ambao ni tunu ya Taifa letu idumu lakini pia uwepo wa mashirikiano na kukaa kwa pamoja kama ndugu kusikilizana pale kwenye matatizo na pale palipo na shida ama matatizo tuone namna gani ya kuyashughulikia." Amesema Kardinali Rugambwa.
Kiongozi huyo wa dini nchini Tanzania ameongeza pia kwamba kuombea amani ni maelekezo ya Baba Mtakatifu wa Kanisa Katoliki duniani Papa Leo, ambaye amekuwa akionesha kwa vitendo namna ambavyo amekuwa akishirikiana na Viongozi wa dini nyingine kukaa na kusali pamoja kwa kukuza imani zao kwa Mungu mmoja ambaye kila muumini wa dini amekuwa akimuamini pamoja na kuimarisha na kukuza maridhiano miongoni mwa jamii sambamba na kuombea amani.
Mwisho.








0 Comments