NA CHAUSIKU SAID, MATUKIO DAIMA MWANZA.
WAKATI uchaguzi mkuu ukikaribia, vijana nchini Tanzania wameombwa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika zoezi la kupiga kura, huku wakisisitizwa kudumisha amani ambayo imekuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya taifa.
Haya yamebainishwa na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, katika kongamano la vijana lililofanyika Jijini Mwanza, huku kongamano hilo likilenga umuhimu wa vijana Kushiriki katika uchaguzi.
Nyalandu alisisitiza kuwa uchaguzi ni tukio la kipekee na la kihistoria, ambalo linatufanya tuonekane mbele ya mataifa mengine kama Taifa linalozingatia demokrasia, utulivu, na amani.
“Siku ya kupiga kura ni siku takatifu, ni siku ambayo Tanzania inawaonesha mataifa mengine kuwa Taifa lenye amani, utulivu, na mifumo ya demokrasia inayojali misingi na tunu zetu," alisema Nyalandu.
Aidha amesisitiza kuwa Nchi ya Tanzania ni kivutio cha wivu kwa watu wa mataifa mengine, kutokana na amani na utulivu iliyonayo.
“Hii ni amani ya kipekee ambayo tunapaswa kuiheshimu na kuilinda kwa gharama yoyote,” aliongeza Nyalandu.
Katika kongamano hilo, vijana walijizatiti kuelezea umuhimu wa kushiriki katika uchaguzi kama sehemu ya haki zao za kiraia na wajibu wao kwa taifa.
Pendo Mshota mmoja wa vijana waliohudhuria katika kongamano, ameeleza kuwa vijana ndio nguzo muhimu ya taifa hivyo wanapaswa kujitokeza kwenye zoezi la kupiga kura oktoba 29 Mwaka huu.
“Sisi vijana tunayo nafasi kubwa ya kubadili hatima ya nchi yetu kwa kuchagua viongozi bora," alisema Msote. "Hatutaki kuona amani yetu inavunjwa, na kwa hiyo ni muhimu kushiriki katika uchaguzi kwa wingi.”
Kashinje John alifafanua kuwa kura ni sauti ya kila mmoja, na ni wajibu wa kijana kuhakikisha kuwa anaitumia vizuri katika Kushiriki katika uchaguzi.
"Kura yako ni sauti yako, na ni njia ya kuwakilisha wale ambao hawana fursa ya kupiga kura. Kura yako moja inahusika na mustakabali wa taifa letu na wa wale wote ambao hawakuwa na nafasi ya kushiriki," alisema Kikuweli.
Vijana pia walisisitizwa kuhusu umuhimu wa kulinda amani. “Amani ni urithi wetu. Hii amani tuliyonayo, tunaweza kuiona kama ni ya kawaida, lakini ni thamani kubwa na hatupaswi kuichezea,” alieleza Kikuweli.
Katika muktadha wa kisheria, Ibara ya 74 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasisitiza kuanzishwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi, ambayo ina jukumu la kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa njia ya haki, huru, na kwa amani. Kura ni haki na ni wajibu wa kila mtanzania, hususan vijana, kuchangia katika kuunda taifa bora.
Mwisho.
![]() |











0 Comments