Na Ashrack Miraji Matukio Daima
Taasisi ya Tanzania Jumuishi (TAJU) imewataka Watanzania wote kuhakikisha uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu unakuwa wa amani, ikisisitiza kuwa watu wenye ulemavu ndio waathirika wakubwa zaidi wakati wa vurugu na machafuko ya kisiasa.
Katibu Mkuu wa TAJU, Innocent Siliwa, amesema taasisi hiyo iliyoanzishwa na kusajiliwa na watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali, imekuwa ikishuhudia katika mataifa mengine jinsi chaguzi zinavyoweza kugeuka chanzo cha machafuko na uvunjifu wa amani.
Kwa kutambua hali hiyo, Siliwa alisema TAJU imechukua hatua za makusudi za kuombea amani nchini ili Tanzania iendelee kuwa kisiwa cha utulivu. na watu wenye ulemavu wanahitaji amani zaidi kuliko makundi mengine yote katika jamii kwa sababu wao ndio waathirika wa kwanza pindi vurugu zinapotokea.
Tushiriki uchaguzi kwa amani, tusijihusishe na vitendo vya uhalifu au vurugu. Viongozi tunaowachagua ni viongozi wa kijamii, si wa chama. Chama ni tiketi tu ya kupata nafasi ya kutuhudumia,” alisema Siliwa.
Aidha, amewataka wasimamizi wa uchaguzi, viongozi wa vyama na wagombea wote kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa uadilifu ili kila mshiriki aridhike na matokeo
Amesema uwazi na weledi katika usimamizi wa uchaguzi utasaidia kudumisha amani na umoja wa taifa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TAJU, Mhe. Ndonge Said Ngonge, alisema kikao cha watu wenye ulemavu kilichoratibiwa na taasisi hiyo kiliitishwa mahsusi kwa ajili ya kukabidhi uchaguzi huo kwa Mwenyezi Mungu, ili amani iendelee kutawala nchini.
“Kikao hiki hakina itikadi ya chama chochote, bali kina itikadi ya amani na utu wetu kama watu wenye ulemavu,” alisema Ngonge.
Ngonge aliongeza kuwa watu wenye ulemavu pia ni washiriki kamili wa uchaguzi wa viongozi kuanzia ngazi ya urais hadi madiwani, na kwamba wapo walemavu kadhaa waliogombea nafasi kupitia vyama mbalimbali kama vile CUF na Chama cha Makini.
Aidha, aliwahimiza makundi yote ya kijamii — wanawake, vijana, wazee na walemavu — kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura na kushiriki katika utulivu.
“Sisi watu wenye ulemavu tupo na tumetokana na jamii ileile isiyo na ulemavu. Amani ya taifa hili ni urithi wa wote, tusiiweke rehani,” alisisitiza.
Mmoja wa washiriki wa mkutano huo, Asha Kikala, alisema amejipanga vizuri kuelekea siku ya kupiga kura na amewataka Watanzania wenzake kutoshiriki katika uchochezi au vitendo vya uvunjifu wa amani.
“Tukivuruga uchaguzi, tutaleta madhara makubwa kwetu sisi wenye ulemavu. Tukumbuke hatuna nchi nyingine ya kwenda,” alisema Kikala.
Kwa ujumla, TAJU imewataka Watanzania wote kulinda amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi, ikisisitiza kuwa amani ndiyo tiba na kinga ya kweli kwa watu wenye ulemavu na kwa taifa kwa ujumla.











0 Comments