Na Moses Ng’wat, Mbozi.
KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ismail Ali Ussi, amewataka wananchi wa Wilaya ya Mbozi kuunga mkono jitihada za Serikali katika ujenzi wa miradi ya maendeleo.
Akizungumza na wananchi wa Kata ya Hasamba, wilayani Mbozi mara baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa barabara ya VETA kwa kiwango cha changarwe yenye urefu wa kilomita 1.8, alisema serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipanga kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora bila ubaguzi.
“Maendeleo yanayoshuhudiwa hapa ni juhudi za Serikali ya Dkt. Samia kuhakikisha kila mwananchi, bila kujali nafasi yake, ananufaika na miradi ya maendeleo,” alisema Ussi na kuongeza kuwa amejiridhisha kwa asilimia 100 na ubora wa kazi ya mradi huo.
Barabara hiyo inajengwa kwa gharama ya Sh milioni 115.8 kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri ya Mbozi, ambapo inatarajiwa kurahisisha usafiri wa wanafunzi na wakufunzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) na Chuo cha Uuguzi Mbozi, pamoja na kuunganisha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Songwe.
Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Hamad Mbega, alisema lengo kuu la mradi huo ni kumuunga mkono Rais Dkt. Samia baada ya kutoa kiasi cha Sh bilioni 6.5 za ujenzi wa chuo cha VETA .
“Barabara hii siyo tu itasaidia taasisi, bali pia ni nyenzo ya kuchochea maendeleo ya wananchi, hasa kwenye usafirishaji wa mazao kama mahindi, kahawa, mbogamboga na mazao mengine kutoka mashambani kwenda viwandani, maghalani na masokoni,” alisema Mbega.
Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Mbozi, Mhandisi Lyoki Mwita, alisema mradi huo ni sehemu ya mkataba wa ujenzi wa jumla ya barabara tatu zenye urefu wa kilomita 3.85 kwa gharama ya Sh milioni 214.3.
Alizitaja barabara nyingine kuwa ni barabara ya Mwenge (km 1) yenye thamani ya Sh milioni 67.1 na barabara ya Old Vwawa (km 1) yenye thamani ya Sh milioni 38.1.
Mhandisi Mwita alisema mradi unatekelezwa na kampuni ya S.A Investment Limited, ambapo tayari kazi za kufukia mifereji, kuchimba mifereji ya maji ya wazi (km 0.57) na kuweka tabaka la changarwe kwa kilomita 1.70 kati ya 1.85 zimekamilika.
“Hadi sasa mkandarasi amelipwa Sh milioni 51.3 kwa kazi zilizotekelezwa,” alisema Mwita.
Mwisho.
0 Comments