Header Ads Widget

TDB KUWEKA VITUO VYA MAZIWA KATIKA SHULE ZOTE NCHINI IFIKPO 2026


Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma

BODI ya Maziwa Tanzania (TDB) imetangaza mpango wa kuhakikisha shule zote nchini zinakuwa na vituo vya maziwa ifikapo mwaka 2026 ikiwa ni jitihada za kuendeleza unywaji wa maziwa mashuleni na kuboresha lishe kwa watoto

Akizungumza na waandishi wa habari Goerge Msalya Msajili bodi ya Maziwa Tanzania TBD  katika ofisi za bodi kabla ya  kuelekea maadhimisho ya Siku ya Maziwa Duniani ambayo hufanyika kila jumatano ya mwezi wa tisa ambapo maadhimisho hayo mwaka huu yalifanyika  kitaifa mkoani wa Geita .

Msajili huyo wa TDB amesema tayari shule 154 zinahudumiwa kwa kupewa maziwa mara tatu kwa wiki huku lengo likiwa ni kufikia shule 5000 katika kipindi kifupi kijacho

Amesema kupitia ushirikiano na Serikali chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi bodi hiyo inaendesha mpango wa kuhakikisha kila shule nchini inafikiwa na huduma ya maziwa ambapo zaidi ya shilingi bilioni 28 zinahitajika kufanikisha malengo hayo. 

"Katika mkoa wa Dodoma tayari vituo viwili vya maziwa vimeanzishwa mashuleni kama sehemu ya maandalizi ya utekelezaji wa mpango huo kitaifa huku TDB ikisisitiza kuwa maziwa ni mlo kamili unaochangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa mtoto na ustawi wa afya ya jamii, " Amesema msajili huyo

Msalya amesema maziwa pia ni chanzo kikubwa cha ajira na uchumi ambapo sekta hiyo inachangia asilimia mbili ya pato la taifa na inatoa ajira kwa zaidi ya watu milioni sita nchini hali inayoonesha kuwa uwekezaji kwenye maziwa una manufaa mapana kwa taifa

" Ukweli ni kwamba Bado unywaji wa maziwa nchini unasuasua hali inayosababishwa na ukosefu wa elimu ya kutosha kuhusu umuhimu wa maziwa pamoja na mila na mitazamo potofu kuwa maziwa hayana faida hali inayowafanya baadhi ya wazazi kutowapa watoto wao maziwa mara kwa mara, " Amesema Msajili huyo

Aidha Msajili huyo ameitaka jamii kuacha tabia ya kutumia chupa za plastiki zilizotumika awali kama vile za maji kwa ajili ya kubebea maziwa kwa kuwa huweza kusababisha madhara makubwa kiafya yakiwemo magonjwa sugu kama kansa badala yake imeshauri maziwa yahifadhiwe kwenye vyombo salama vya chuma au aluminiam vilivyooshwa kwa maji ya moto

"Kwa sasa bodi inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya maziwa kuhamasisha ulaji wa maziwa nchini kwa kuandaa kampeni maalum zenye lengo la kuwajengea wananchi utamaduni wa kunywa maziwa kila siku kuanzia utotoni hadi ukubwani ili kuhakikisha afya bora na maendeleo endelevu ya jamii, "Amesema Msalya

Maadhimisho ya Siku ya Maziwa Duniani mwaka huu yalipewa uzito wa kipekee kwa kuwa ni fursa ya kutoa elimu kuhusu lishe bora ambapo watoto walipewa kipaumbele kikuu kutokana na changamoto ya utapiamlo inayolikabili taifa na hivyo bodi hiyo kuona umuhimu wa kufikisha maziwa katika kila shule ili kuimarisha afya za wanafunzi na kukuza uchumi wa ndani kupitia soko la maziwa

Hata hivyo Tanzania haiwezi kuwa na kizazi chenye afya bora bila kuhakikisha watoto wanapata mlo kamili unaojumuisha maziwa na kwamba mafanikio ya mpango huo yatatokana na ushirikiano wa karibu kati ya serikali sekta binafsi na wananchi kwa ujumla

Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI