Header Ads Widget

ALIYEKUWA RAISI WA UFARANSA NICOLAS SARKOZY AANZA KUTUMIKIA KIFUNGO GEREZANI

 

Rais wa zamani wa Ufaransa Nicolas Sarkozy leo ameanza kutumikia kifungo cha miaka mitano gerezani baada ya kuhukumiwa kwa uhalifu wa kula njama ya kufadhili uchaguzi wa mwaka 2007 kinyume na sheria kwa kutumia fedha zilizotoka kwa aliyekuwa kiongozi wa Libya Muamar Gaddafi.

Bwana Sarkozy mwenye umri wa miaka 70 aliwasili leo asubuhi katika jela la La Sante mjini Paris akisindikizwa na mkewe Carla Bruni na kushangiliwa na wafuasi wake walioimba wimbo wa taifa.Kupitia ukurasa wake wa X,Kiongozi huyo amedai ni muathiriwa wa chuki na visasi na kuongeza kuwa anayefungwa leo gerezani sio rais wa zamani wa Ufaransa bali mtu asiye na hatia.

Amekuwa akikanusha mara kwa mara kuhusika na makosa yoyote yanayohusiana na ufadhili wa uchaguzi wa 2007.

Sarkozy ambaye alikuwa Rais wa Ufaransa kati ya mwaka 2007 hadi 2012,atakuwa rais wa zamani wa Ufaransa kufungwa jela tangu Marshal Philipphe,aliyekuwa kiongozi wa Ufaransa aliyekuwa na mafungamano na utawala wa kinazi kufungwa baada ya vita vya pili vikuu vya dunia.

Sebastien Cauwel,mkuu wa gereza atakalofungwa bwana Sarkozy amesema kiongozi huyo atafungwa kwenye seli yake pekee, tofauti na wafungwa wengine lakini ataweza kutumia uwanja wa kufanyia mazoezi mara mbili kwa siku akiwa pekee yake kwasababu za kiusalama.

Seli atakayokuwa kama seli nyingine za jela hiyo ina bafu,ataweza kuwa na televisheni ikiwa atalipia euro 14 kwa mwezi na simu.

Wakili wake Jean Michel Darrois amesema mteja wake anajiandaa kuelekea gerezani leo na atabeba fulana kadhaa atakazovaa kukiwa na baridi na viziba masikio kwani gerezani huenda kukawa na kelele nyingi.

Sarkozy pia aliwaambia waandishi habari atabeba vitabu vitatu kikiwemo Count of Monte Cristo ambacho kinasimulia mtu aliyefungwa jela kwa njia za kionevu na kupanga jinsi ya kulipiza kisasi dhidi ya waliomsaliti.

Baada ya miaka mingi ya vuta nikuvute za kisheria kuhusu madai kuwa timu yake ya kampeini kuwa ilipokea mamilioni ya fedha kutoka kwa aliyekuwa kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi,Sarkozy hivi karibuni alihukumiwa kifungo hicho cha miaka mitano jela.

Licha ya Sarkozy kupatikana na hatia ya kushirikiana na washirika wake wa karibu kupokea fedha kinyume na sheria,aliondolewa makosa ya yeye mwenyewe binafsi kupokea fedha hizo au kuzitumia.

Amekuwa akisisitiza kuwa kesi dhidi yake imechochewa kisiasa akisema majaji wamekuwa wakitaka kumdhalilisha.

Amekata rufaa dhidi ya hukumu dhidi yake lakini kuambatana na sheria za Ufaransa kuhusu hukumu inayomkabili,inamaanisha kuwa sharti ewekwe gerezani anaposubiri rufaa yake ishughulikiwe.

Hukumu hiyo imezua ghadhabu miongoni mwa washirka wake wa kisiasa na wafuasi wa vyama vya mrengo wa kulia wenye misimamo mikali.

Kulingana na uchunguzi wa maoni ya wananchi,asilimia 58 ya wafaransa wanaamini kuwa hukumu dhidi ya rais wao wa zamani haikutokana na upendeleo wowote na asilimia 61 ya waliohojiwa wanaunga mkono uamuzi wa kumfunga jela bila ya kusubiri uamuzi wa mahakama ya rufaa.

Rais Emmanuel Macron ambaye amekuwa na mahusiano mazuri na Bwana Sarkozy na mkewe Carla Bruni amesema alikutana na Sarkzi kabla ya kuanza hukumu yake na waziri wa sheria Gerald Darmanin ambaye pia yuko karibu na Sarkozy,amesmea atakwenda kumtembelea kiongozi huyo akiwa gerezani.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI