Watalii wa ndani na nje ya Tanzania sasa wataweza kupata taarifa zote muhimu kuhusu hifadhi za taifa na vivutio vya utalii nchini kwa urahisi zaidi kupitia programu tumizi mpya iliyopewa jina la Tanapa Go, iliyozinduliwa rasmi na Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, katika Hifadhi ya Taifa ya Mikumi.
App hiyo inawawezesha watumiaji kuona taarifa za hifadhi 21, maeneo matano ya malikale, vivutio, gharama, ramani, na ratiba za huduma,vyote kupitia simu zao za mkononi.
“Teknolojia hii itasaidia kuondoa kikwazo cha taarifa na lugha. Dunia sasa ipo kiganjani, hivyo hii ni njia mpya ya ‘marketing with selling’ inayoweka Tanzania kwenye ramani ya utalii wa kisasa,” alisema Dkt. Abbasi.
Aliongeza kuwa Serikali inaendelea kuboresha miundombinu kwenye hifadhi, ikiwemo viwanja vya ndege vya kisasa vya Mikumi, Ruaha na Nyerere, ambavyo vinaelekea kukamilika, hatua itakayowezesha wageni kufika kwa urahisi zaidi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Tanapa, Jenerali Mstaafu George Waitara, alisema ubunifu huo ni kielelezo cha kasi ya mageuzi katika sekta ya uhifadhi na utalii nchini.
Mkurugenzi wa Masoko kutoka Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Rahma Sanya, aliongeza kuwa ushirikiano kati ya Zanzibar na Bara umeimarika, huku asilimia 70 ya watalii wa Mikumi wakitoka Zanzibar.
Akashauri maboresho mbalimbali kufanyika kuvuta zaidi watalii kama alivyoelewa na wadau wa sekta hiyo ikiwemo kuongeza huduma za ndege kutoka Zanzibar kuja kwenye Hifadhi bara, kuboreshwa miundo mbinu ya viwanja vya ndege hifadhini na malazi kwaajili ya wageni hasa kwa hifadhi kama Mikumi ambayo imekuwa rahisi kwa wageni kuja na kuondoka kutokea Zanzibar.
Naibu Kamishna wa Uhifadhi Tanapa, Masana Mwishawa, alisema kuzinduliwa kwa Tanapa Go pamoja na jarida jipya la Tanapa ni hatua ya kimkakati ya kukuza mwamko wa utalii wa ndani na kuongeza mapato yatakayochangia uchumi wa Taifa.
Naibu Kamishna wa Uhifadhi Tanapa, Masana Mwishawa, alisema kuzinduliwa kwa Tanapa Go pamoja na jarida jipya la Tanapa ni hatua ya kimkakati ya kukuza mwamko wa utalii wa ndani na kuongeza mapato yatakayochangia uchumi wa Taifa.
0 Comments