Na Hamida Ramdhan,Matukio Daima Media Dodoma
MGOMBEA udiwani Kata ya Ipagala Danson Kaijage kupitia tiketi ya Chama cha ACT.Wazalendo amehaidi kutafuta wataalamu wa masuala ya biashara kwa ajili ya kutoa elimu kwa akina mama,Vijana na watu wenye mahitaji maalumu ili waweze kuwa na ufahamu mkubwa wa kuomba mikopo ya Halmashauri.
Ametoa kauli hiyo katika mikutano ya siasa inayoendelea katika kata hiyo ya kuomba ridhaa ya kuchaguliwa kuwa Diwani wa kata ya Ipagala ambayo imakabiliwa na changamoto ya akina mama,Vijana na Watu wenye mahitaji maalumu kushindwa kupata mikopo hiyo ya halmashauri.
Mgombea huyo alieleza kuwa halmashauri ya Jiji la Dodoma imekuwa ikihamasisha makundi hayo kuanzisha vikundi ili vipate mikopo lakini hakuna mwitikio kutokana na kutokuwa na uelewa wa kutosha katika kuanzisha vikundi na kuvisajili.
"Nataka kuwaeleza ndugu zangu wana Ipagala kama mtanipa ridhaa ya kuwa Diwani wa kata hii nitahakikisha namtafuta mtaalamu wa kuandika andiko la miradi na kunzisha madarasa ya ujasiliamali ili iwe rahisi kuanzisha vikundi vya kukopa mikopo ya halmashauri ya asilimia 10.
"Pia nitahitaji kukaa na wenyeviti wa mitaa yote nane ili kuona maeneo ambayo ni ya wazi ili yaweze kutumiwa na wajasiliamali wadodo wadogo kwa kuanzisha viwanda vidogo vidogo"alieleza Kaijage.
Katika hatua nyingine Mgombea huyo ameeleza kusikitishwa kuwepo kwa migogoro ya ardhi katika kata hiyo ambayo inasababisha wananchi kuichukua serikali yao kutokana na vitendo vya dhuruma.
"Kata ya ipagala ni kata ya tatu kutoka zilipo Ofisi za halmashauti ya Jiji ni kati ya kilometa 8 au 9 hivi na ni kata ya tatu kwa maana ya kata ya Viwandani,Kata ya Makole na kufikia kata ya Ipagala.
"Unaweza kuona ukaribu uliopo na wataalamu wapo wanafikika kirahisi nini kinachosababisha kuwepo kwa migogoro ya ardhi katika kata hiyo,naweza kusema kuwa ni viongozi kushindwa kuzingatia mahitaji ya watu ambao waliwachagua"ameeleza Mgombea huyo.
Akizungumzia kuhusu maafisa usafirishaji yaani Boda boda alisema kuwa mpango ni kuwaunganisha kuwa na mfuko wao wa maendeleo ambao unaweza kuwavusha na kuazisha benki yao huku wakijiweka katika hali ya kuaminika na kukopesheka kirahisi na taasisi za kifedha.
Akizungumzia kuhusu masoko amesema ni lazima maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya masoko yafanyiwe kazi ili kutoa fursa kwa wajasiliamali kufanya biashara kwa usalama wao na usalama wa biashara zao.
Katika mikutano yake pia alisema kutokana na umuhimu wa uwepo wa wazee katika kata ya Ipagala akiwa diwani ataongea na mifuko ya Afya ya Jamii ili kuona utaratibu wa kuwakatika bima za afya kwa kushirikisha hata wafadhili ambao ni wapenda maendeleo.
Hata hivyo amewasisitiza vijama,akina mama na marika yote kuhakikisha siku ya tarehe 9 Oktoba wanajitokeza kwa wingi katika vituo vya kupigia kura na kupiga kura na wasisikilize vitisho kuwa siku hiyo itakuwa ya vurugu kwani watanzania ni watu wenye kutaka amani siku zote.
0 Comments