Na Hamida Ramadhani Matukio Daima Media, Dodoma
MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amewataka viongozi wa dini kuendelea kuhimiza amani, mshikamano na utulivu katika jamii, akisisitiza kuwa viongozi hao wana nafasi kubwa katika kuhakikisha hali ya utulivu inaendelea kudumishwa katika mkoa huo unaokua kwa kasi.
Akizungumza jijini Dodoma wakati wa Mwendelezo wake wa kukutana na makundi mabimbali ambapo amekutana viongozi wa dini, na kueleza kuwa serikali inatambua mchango mkubwa wa viongozi wa dini katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi, hususan katika malezi ya kiroho na maadili ya wananchi.
“Kama viongozi wa dini, mnalo jukumu kubwa la kuendelea kuhimiza amani na utulivu tayari tumeanza kuona viashiria vya uvunjifu wa amani, hivyo ni muhimu tukalivalia njuga suala hili kabla hali haijawa mbaya,” amesema Senyamule.
Aidha, ameeleza kuwa kwa miaka ya karibuni, mkoa wa Dodoma umepiga hatua kubwa katika maendeleo, ambapo watu wengi na wawekezaji wameanza kuelekeza macho yao katika mkoa huo, tofauti na hapo awali ambapo Dodoma haikuvutia hata kwa makazi ya kawaida.
“Zamani mtu akisema anakwenda kuishi Dodoma alikuwa anashangazwa. Lakini sasa Dodoma imekuwa kimbilio la watu wengi na wawekezaji tunayo sababu ya kujivunia maendeleo haya, na kuhakikisha tunalinda amani tuliyonayo,” ameongeza.
Senyamule pia alieleza kuwa hadi sasa, wizara 15 tayari zimehamia Mji wa Serikali Mtumba, huku taasisi mbalimbali za serikali zikiendelea na ujenzi wa ofisi na miundombinu pia kukamilika kwa jengo la Mahakama kama ishara ya kukua kwa mji huo.
Katika hatua nyingine, Senyamule amewataka viongozi wa dini kuhamasisha waumini wao kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi unaotarajiwa kufanyika tarehe 29 Oktoba, akisisitiza umuhimu wa kutumia haki yao ya kikatiba.
“Haki ya kupiga kura ni haki ya kikatiba na kidemokrasia wahimizeni waumini wenu wajitokeze kwa wingi kuchagua viongozi wanaowataka kwa miaka mitano ijayo,”amesema .
Hata hivyo alishukuru viongozi wa dini kwa kuendelea kushirikiana na serikali katika masuala mbalimbali ya maendeleo ya mkoa wa Dodoma.
Akiongea kwa niaaba ya viongozi wenzake katika kikao hicho Msemaji kutoka Ofisi ya Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Dkt, Ahmed Saidi, amesema kama viongozi wataendelea kuomba ni dua nchi iendelee kubaki na amani na utulivu.
"Tukumbuke amani ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na ni msingi wa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla, "Amesema
Amesema wanaendelea kuelimisha jamii juu ya elimu ya amani, kuelewa maana yake, thamani yake, na athari kubwa zitakazotokea pale ambapo amani itatoweka.
" Bila amani, hakuna maendeleo, hakuna mshikamano, na hakuna maisha bora. Kila mmoja wetu ana jukumu la kuitunza na kuilinda amani kama tunavyolinda maisha yetu, "Amesema msemaji huyo
0 Comments