Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro Alex Mkama
Na Lilian Kasenene, Morogoro
JESHI la Polisi mkoa wa Morogoro limewahakikishia wananchi kuwa usalama upo wa kutosha na vyombo vyote vya ulinzi na usalama vimejiandaa kukabiliana na yeyote atakayethubutu kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro Alex Mkama alisema hayo alipozungumza na Waandishi wa Habari.
Mkama alisema Jeshi hilo linaendelea na majukumu yake kwa kufuata miongozo ya kisheria huku doria mahususi za kuandaa mazingira Salama kwa ajili ya kufanya uchaguzi mkuu Oktoba 29,2025.
Aidha kamanda huyo alisema wananchi hawapaswi kuogopa muonekano wa vyombo vya usalama bali waichukue kama fursa ya kutimiza jambo hilo kikatiba.
"Mambo yanayozuiliwa ni pamoja uhamasishaji wa maandamano, uhujumu wa miundombinu ya uchaguzi,uhujumu wa miundombinu mbalimbali, ufungaji wa barabara, kujeruhi au ghasia ya aina yoyote ambayo inatafsiliwa kuwa ni jaribio la kuvuruga amani," alisema kamanda Mkama
Jeshi hilo la Polisi likatoa onyo kwa wale wote watakaojaribu kutaka kufanya maandamano au kuzuia wananchi wasishiriki zoezi la upigaji kura kuwa wataadhibiwa kwa mujibu wa Sheria.
Mkazi wa Manispaa ya Morogoro Nicolaus John alisema wanachoomba ni usalama kuzingatiwa kwani vitisho vimekuwa vingi kila mmoja anasema kivyake,Polisi wawe mbali na vituo vya kupigia kura wakiwa karibu wanaweza kupata uwoga wa kwenda kwenye kituo kupiga kura.
"Polisi wawepo walinde lakini wasiwe karibu zaidi wawe kwa mbali wakati mwingine mtu anakuwa na nia ya kwenda kupiga kula anapowaona askari tu pale kituona anakuwa mwoga,"alisema Susana Machibya.





0 Comments