Header Ads Widget

PASS,KUIMALISHA UPATIKANAJI WA MITAJI KWA SEKTA YA KILIMO KAGERA.

 

Na Shemsa Mussa -Matukio Daima 

Kagera.

Katika kuadhimisha miaka 25 ya huduma kwa wakulima na wafugaji, PASS Trust imeandaa jukwaa maalum kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na taasisi za fedha nchini, ili kukuza upatikanaji wa mitaji kwa wadau wa sekta ya kilimo, uvuvi, mifugo na mazao ya misitu.


Akizungumza katika semina iliyowakutanisha wadau hao, Mkurugenzi wa Biashara wa PASS Trust, Bw.Adam Kamanda, amesisitiza umuhimu wa taasisi za kifedha kuendelea kushirikiana na PASS Trust katika kufungua fursa zaidi za uwezeshaji kwa wakulima, hususan wanaojihusisha na uzalishaji wa mazao ya Kanda ya Ziwa.

“Taasisi za kifedha zina nafasi ya kipekee katika kusaidia wakulima kuongeza tija na thamani ya uzalishaji. Kupitia ushirikiano na PASS, tunaweza kuwafikia wakulima wengi zaidi na kuwapa mitaji wanayohitaji kwa masharti nafuu,” amesema Bw ,Kamanda.

Aidha, ameeleza kuwa jukwaa hilo ni sehemu ya juhudi endelevu za PASS Trust katika kuhakikisha kuwa wakulima wadogo na wakubwa wanakuwa sehemu ya uchumi jumuishi na endelevu.

Kwa mujibu wa PASS Trust, lengo kuu la jukwaa hilo ni kujenga majadiliano yenye tija kati ya taasisi za kifedha na wadau wa kilimo, ili kuibua mbinu bora za kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa sekta zisizo rasmi, ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikikumbwa na changamoto za mitaji.


Jukwaa hili ni miongoni mwa matukio muhimu katika kuadhimisha miaka 25 ya PASS Trust, ikiwa ni kielelezo cha dhamira ya taasisi hiyo katika kuendeleza ushirikiano wa kimkakati na wadau mbalimbali kwa ajili ya kukuza sekta ya kilimo nchini.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI