Na Shemsa Mussa -Matukio Daima
Kagera.
Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Watumishi wa Umma Bukoba na Missenyi (BURUTE SACCOS) kimetimiza kwa vitendo Msingi wa Saba wa Ushirika unaohimiza vyama vya ushirika kujali na kusaidia jamii inayowazunguka.
Akizungumza katika hafla maalum ya utoaji wa msaada kwa jamii, Mwenyekiti wa BURUTE SACCOS, Mwalimu Charles Tegamaisho, amesema chama hicho kimejipambanua kuwa si tu chombo cha kuweka na kukopa, bali pia ni mshirika muhimu wa maendeleo ya kijamii katika mkoa wa Kagera.
“Misingi saba ya ushirika ndiyo nguzo ya utendaji wetu, na leo tunatekeleza msingi wa saba – kujali jamii – kwa vitendo. Tumeamua kugawa sehemu ya mapato yetu ili kusaidia katika sekta muhimu kama elimu na afya,” alisema Mwalimu Tegamaisho.
Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mheshimiwa Fatma Mwassa, ambaye alikuwa mgeni rasmi, BURUTE SACCOS ilitoa msaada wa Madawati 340, Vyandarua 205 pamoja na Mashuka 240.
Vilevile, vifaa kama pampasi za watoto chini ya miaka mitano (boksi 6) sukari kilo 100 maharage kilo 200pamoja na bima za afya kwa wanafunzi 40 vilitolewa.
Msaada huo umelenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuimarisha huduma za afya katika jamii za Bukoba na Missenyi.
Akizungumza wakati akikabidhi vifaa hivyo kwa wahusika, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe,Hajjat Fatma Mwassa, ameipongeza BURUTE SACCOS kwa kuwa mfano wa kuigwa katika kutekeleza falsafa ya ushirika.
“Huu ni ushahidi kwamba vyama vya ushirika vinaweza kuwa nguvu ya maendeleo ya watu na si ya wanachama pekee. Nawaomba SACCOS nyingine ziige mfano huu wa kujali jamii,” alisema Mheshimiwa Mwassa.
BURUTE SACCOS imeendelea kuwa nguzo muhimu kwa watumishi wa umma katika maeneo ya Bukoba na Missenyi, ikichochea ustawi wa kifedha wa wanachama wake na kuchangia maendeleo ya kijamii katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kagera.
0 Comments