Mjumbe maalum wa Marekani Steve Witkoff na mkwe wa Rais wa Marekani Donald Trump, Jared Kushner watajiunga na mazungumzo ya mpango wa amani wa Gaza kati ya wapatanishi wa Israel na Hamas nchini Misri siku ya Jumatano.
Kuwasili kwao kunakuja wakati siku ya pili ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja Jumanne ilimalizika bila matokeo yanayoonekana, afisa mkuu wa Palestina anayefahamu mazungumzo hayo aliiambia BBC.
Trump alitoa maoni siku ya Jumanne, wakati Israel ikiadhimisha kumbukumbu ya mwaka wa pili wa mashambulizi ya Oktoba 7 ya Hamas, akisema "kuna uwezekano kwamba tunaweza kuwa na amani Mashariki ya Kati".
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu hakuzungumzia hali ya mazungumzo hayo, lakini aliwaambia Waisraeli kuwa walikuwa katika "siku mbaya za uamuzi".
Katika chapisho kwenye X, Netanyahu aliongeza kuwa Israel itaendelea kuchukua hatua ili kufikia malengo yake ya vita: "Kurejea kwa wote waliotekwa nyara, kuondolewa kwa utawala wa Hamas na ahadi kwamba Gaza haitakuwa tishio tena kwa Israel".
Witkoff na Kushner walitarajiwa kuondoka Marekani Jumanne jioni na kuwasili Misri siku ya Jumatano, chanzo kinachofahamu kuhusu mazungumzo hayo kiliiambia BBC.
0 Comments