Na Shemsa Mussa -Matukio Daima
Kagera.Mgombea wa nafasi ya Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya mkutano wa kampeni katika Uwanja wa Kaitaba, Manispaa ya Bukoba, Mkoa wa Kagera. Katika hotuba yake, Dkt. Samia amewaeleza wananchi kuhusu utekelezaji wa ahadi zilizopo katika Ilani ya CCM, pamoja na mipango ya kuwaletea maendeleo katika sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Dkt. Samia amewaeleza kuwa serikali ya CCM itaendelea kuboresha huduma za jamii ili kila mwananchi apate huduma kwa urahisi. Aidha, amewaeleza kuwa huduma ya bima ya afya itasaidia kugharamia matibabu pamoja na gharama za huduma endapo mgonjwa atafariki dunia.
Katika sekta ya elimu, ameahidi kuwa wanafunzi wanaomaliza kidato cha sita watawezeshwa kupata mikopo ili kujiunga na vyuo vikuu, hatua ambayo inalenga kuongeza usawa wa fursa za elimu ya juu kwa Watanzania wote.
Kwa upande wa nishati, Dkt. Samia ametangaza mpango wa kujenga vituo vya kupokea na kupoza umeme ili kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika kipindi chote cha mwaka.
Kuhusu sekta ya uvuvi, ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo, serikali itatoa mafunzo na vifaa kwa wavuvi, pamoja na kuwawezesha vijana kufuga samaki kwa kutumia vizimba, ili kukuza uchumi wa bahari.
Vilevile, ameahidi kujenga machinjio ya kisasa ili kuboresha ufugaji wa ng’ombe na kuinua kipato cha wafugaji wa Mkoa wa Kagera.
.jpeg)
Pia, aligusia suala la mafuriko yanayoikumba Manispaa ya Bukoba na kueleza kuwa serikali itajenga kingo za mto Kanoni ili kuzuia madhara yanayosababishwa na mafuriko hayo.
Katika kumaliza mkutano wake wa mwisho wa kampeni kwa Mkoa wa Kagera, Dkt. Samia Suluhu Hassan amewaomba wananchi wa mkoa huo kumpigia kura ili aendelee kuwatumikia na kuwaletea maendeleo endelevu.
0 Comments