Header Ads Widget

SORECU YATUMIA MICHEZO KUHAMASISHA MATUMIZI YA NISHATI SAFI NA MAPAMBANO DHIDI YA MABADILIKO YA TABIA NCHI.

 

Na Moses Ng'wat, Mbozi.

Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Songwe (SORECU) kimeendelea na kampeni ya kupambana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kutumia michezo kama jukwaa la kutoa elimu kwa vijana juu ya matumizi ya nishati safi, ikiwemo umuhimu wa  kujiunga katika vyama vya ushirika.

Akizungumza katika kilele cha Bonanza la Michezo la Songwe, lililofanyika katika viwanja vya CCM Vwawa, wilayani Mbozi, Ofisa Oparesheni wa SORECU, Moni Mwampamba, amesema bonanza hilo lililoanza Oktoba 10, 2025, lina lengo la kuhamasisha vijana kutumia nishati safi, kulinda mazingira, na kushiriki katika shughuli za kilimo na ushirika.

"Tunatoa elimu ya matumizi ya nishati safi kama gesi, umeme na mkaa mbadala ili kupunguza uharibifu wa misitu na kulinda vyanzo vya maji, hii ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati wetu wa 2024–2027 wa kuimarisha ushirika, tukilenga kuongeza ushiriki wa vijana katika shughuli za kilimo na ushitika,” amesema Mwampamba.

Ameongeza kuwa, kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, vijana wanaunda zaidi ya asilimia 34 ya Watanzania, hivyo ni kundi muhimu katika kuendeleza kilimo endelevu na matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Jabiri Omary Makame, ambaye alikuwa mgeni rasmi, amesema mabadiliko ya tabia nchi yanasababishwa kwa kiasi kikubwa na shughuli za kibinadamu kama uchomaji wa misitu na matumizi ya kuni pamoja na mkaa wa miti.

"Tunawahamasisha wananchi wote wa Songwe kugeukia nishati safi kama umeme, gesi na mkaa wa makaa ya mawe ambao unapatikana katika wilaya za Ileje na Mbozi".


"Kwa sasa vijiji vyote vimepatiwa umeme, na tunakamilisha vitongoji vilivyobaki — hivyo hakuna sababu ya kuendelea kutumia kuni na mkaa wa miti,” amesisitiza Makame.

Bonanza hilo ni sehemu ya jitihada za SORECU kuunganisha vijana kupitia michezo na elimu ya uhifadhi wa mazingira, ili kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara bila kuathiri ekolojia ya mkoa huo.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI