NA MATUKIO DAIMA.
Mgombea Ubunge Jimbo la Ngara kupitia Chama cha Mapinduzi CCM ndugu Dotto Jasson Bahemu amemuomba Dkt. Samia Suluhu Hassan mgombea nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kujenga kituo kipya cha Mabasi mjini Ngara.
Dotto Jasson Bahemu ambaye ni mgombea pekee wa Ubunge Jimboni la Ngara amewasilisha ombi hilo kwa niaba ya wananchi wa Ngara kupitia mkutano wa Kampeni wa Mgombea nafasi ya Urais kupitia Chama cha Mapinduzi Dkt Samia Suluhu uliofanyika Wilayani Karagwe.
Amesema, kujengwa kwa stendi mpya ya mabasi mjini Ngara kutachochea maendeleo ya Wilaya hiyo na kufungua fursa mbalimbali za biashara.
Katika hatua nyingine,amemueleza mgombea huyo ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Ngara ni moja ya wilaya zinazozalisha zao la Parachichi, kwa wingi.
Amemuomba Rais Dokta Samia Suluhu Hassan atakapopata ridhaa ya kuchaguliwa, awasaidie wakulima kwa kuwajengea jengo maalum lenye vyumba vya baridi (Cord Room) kwa ajili ya kuhifadhi matunda ya Parachichi kabla ya kusafirishwa.
Ombi lingine lililowasilishwa na Bahemu kwa Dkt. Samia ni ujenzi wa Barabara mpya ya Lami kutoka Nyakahura,kumubuga,Murusagamba,Keza Rulenge,hadi Murugarama, na Ujenzi wa mradi mpya wa maji kutoka mto Ruvuvu utakaogharimu kiasi cha Shilingi bilioni 41.
Mgombea huyo kijana wa Jimbo la Ngara amesema ikiwa maombi aliyowasilisha yatatekelezwa yataisogeza kasi ya kukua kwa uchumi na Maendeleo ya wananchi wa Wilaya ya Ngara inayopakana na nchi za Rwanda na Burundi
MWISHO.
0 Comments