Na Fadhili Abdallah,Kigoma
WANANCHI wa mkoa Kigoma wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika zoezo la kupiga kura Oktoba 29 mwaka huu ili kuwachagua viongozi wanaowataka sambamba na kuwataka kuzingatia Amani na usalama wanaposhiriki kwenye michakato mbalimbali ya uchaguzi huo unaoendelea.
Shekhe wa mkoa Mwanza,Hassan Kabeke alisema hayo mkoani Kigoma wakati wa matembezi ya Amani ya kidini (Dhafa) ya kuwaombea mashekhe na walimu wakubwa wa dini mkoani Kigoma waliotangulia mbele ya haki sambamba na kuombea uchaguzi mkuu.
Viongozi wa dini mkoani Kigoma wakishiriki matembezi ya kidini (DHAFA) kuombea viongozi wa dini na uchaguzi mkuu
Shekhe Kabeke ambaye ni Mkazi wa Ujiji mkoani Kigoma alisema kuwa Amani ya nchi yetu ni muhimu kuliko jambo lolote hivyo ametaka watanzania wote kushiriki kwenye uchaguzi kwa kuzingatia undugu baina yao badala ya uchaguzi kuwafarakanisha na kuleta vurugu na kuharibu Amani ya nchi.
Kwa upande wake Shekhe wa mkoa Kigoma, Hassan Kiburwa ambaye alishiriki kwenye maandamo hayo amesema kuwa watanzania wanapaswa kuishi kwa kuzingatia misingi ya dini yao ambayo inahimiza upendo, Amani na mshikamano na kwamba mambo hayo ndiyo pekee yanayoweza kutuvusha na kufanya uchaguzi kuwa wa Amani na salama.
Shekhe wa mkoa Mwanza Hassan Kabeke ( wa tatu kulia) akizungumza wakati wa matembezi ya kidini (Dhafa) ya kuombea mashekhe na kuombea uchaguzi Mkuu (wa tatu kushoto) Shekhe wa mkoa Kigoma Hassan Kiburwa
Naye kadhi wa mkoa Kigoma, Muhsin Kitumba amewataka Watanzania kuwaombea dua viongozi wa nchii sambamba na kuombea uchaguzi ufanyike kwa Amani na salama bila vurugu zozote akitaka kukemewa kwa watu wote wenye nia ya kuvuruga uchaguzi na Amani ya nchi.
Maandamano hayo ya kuombea dua Mashekhe na walimu wa dini mkoani Kigoma, kuombea uchaguzi yanaenda sambamba na maulid ya Kumswalia Mtume Muhamad (SAW) ambayo yalitarajia kufanyika katika Msikiti wa ijumaa Kabondo.
Mwisho.
0 Comments