Na Moses Ng’wat, Songwe.
NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Felista Mdemu, amekabidhi pikipiki nane kwa Maofisa Maendeleo ya Jamii mkoani Songwe, huku akiwataka kuongeza bidii, uwajibikaji na ubunifu katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Akizungumza Oktoba 23, 2025, wakati wa hafla ya makabidhiano hayo, Mdemu alisema hatua hiyo inalenga kuboresha utoaji wa huduma za maendeleo ya jamii, hususan katika maeneo ya vijijini ambayo mara nyingi hukabiliwa na changamoto za usafiri.
"Ni matumaini yangu kuwa pikipiki hizi zitakuwa nyenzo muhimu katika kuongeza kasi ya utendaji wenu, kuimarisha mawasiliano na jamii, na kutatua changamoto mnazokutana nazo kazini,” alisema Mdemu.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe, John Mwaijulu, aliishukuru serikali kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya maendeleo ya jamii, akibainisha kuwa vitendea kazi hivyo vitasaidia kufikisha huduma hadi ngazi ya vijiji.
"Hii ni mara ya pili kwa mkoa wetu kupokea pikipiki kutoka serikalini. Awamu ya kwanza tulipokea pikipiki nne zilizogawiwa katika Halmashauri za Ileje na Momba,” alisema Mwaijulu.
Hata hivyo, Mwaijulu alitoa wito kwa Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Mkoa huo kuhakikisha nao kwenye Halmashauri zao wanasaidia vitendea kazi kwa maofisa maendeleo ya jamii ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Naye Ofisa Maendeleo ya Jamii kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, Nelsta Paulo, alisema pikipiki aliyopokea itarahisisha kazi za kuhamasisha wananchi kuibua na kutekeleza miradi ya maendeleo pamoja na kuunda vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, ikiwemo kufuatilia marejesho ya mikopo.
Pikipiki hizo zimegaiwa kwa Maofisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri za Momba, Ileje, Songwe na Mbozi, ambapo kila halmashauri imepata pikipiki mbili.
0 Comments