Na COSTANTINE MATHIAS, Simiyu.
WIZARA ya Kilimo, Bodi ya Pamba, Wakulima na Wadau wengine wa zao la Pamba nchini ikiwemo wanunuzi wa Pamba wamekamilisha maandalizi ya Kilimo cha pamba katika msimu wa 2025/2026 ikiwemo kusambaza mbegu na kugawa Matrekta kwa kuzingatia kalenda ya Kilimo.
Aidha, mafunzo ya kutengeneza mbolea hai kwa Wakulima yameendelea kutolewa katika maeneo mbalimbali ili kuongeza tija na uzalishaji wa zao hilo muhimu la kiuchumi nchini.
Akizungumza na waandishi wa Habari za Pamba, Katibu wa Chama Cha Wanunuzi wa Pamba nchini (TGA), Boaz Ogolla ameipongeza serikali kwa kuleta teknolojia mpya katika sekta ya Pamba jambo ambalo litaongeza tija.
Amesema wakulima wengi wa Pamba wamefundishwa mbinu za kilimo bora, kupima udongo, kudhibiti Wadudu pamoja na kutengeneza mbolea hai ambayo haina gharama kwa mkulima ikiwemo mbolea ya Bio Char na bukasha.
"Tunaipongeza Bodi ya pamba kwa kupeleka mbegu ya Pamba mapema kwa Wakulima, hii ni hatua sababu miaka ya nyuma mbegu ilichelewa... Teknolojia ya kupulizia ya maboza, ndege zisizo na nyuki pamoja na Maafisa Ugani wa BBT ambao wameleta mapinduzi ya kuzalisha kilo Milioni 220 kutoka kilo milioni 149" amesema.
Katibu wa Chama Cha Wanunuzi wa Pamba nchini (TGA), Boaz Ogolla akiongea na waandishi wa Habari za Pamba (hawapo pichani).
Aidha, Ogolla amewaondoa hofu wakulima wa Pamba ambao hawajafikiwa na teknolojia za kilimo kuwa na subira wakati serikali na wadau wa Kilimo wakiendelea kujipanga ili kufikisha huduma hizo za Ugani ili wazalishe kama wakulima wengine.
Alisema kuwa serikali imeanza Mkakati wa kupima Afya ya udongo katika mashamba ya wakulima ili kubaini mahitaji na aina ya mbolea zitakazotumika kwa lengo la kuongeza uzalishaji wenye tija.
Kuhusu uzalishaji wa Pamba hai, Ogolla amesema umeongezeka na kufikia kilo Mil. 30 katika msimu wa kilimo 2024/2025.
Mwisho.







0 Comments