Na Shemsa Mussa -Matukio Daima
Kagera.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kagera limepokea magari matatu kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma za dharura na uokoaji kwa wananchi wa mkoa huo.
Makabidhiano ya magari hayo yamefanyika mjini Bukoba Katika ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Kagera, ambapo Kamanda wa Jeshi hilo, Bw. Joseph Ngonyani, amesema magari hayo ni sehemu ya mpango mpana wa serikali wa kuboresha vitendea kazi kwa vyombo vya ulinzi na usalama nchini.
Bw. Ngonyani amefafanua kuwa kati ya magari yaliyopokelewa, moja ni gari la wagonjwa litakalotumika kusafirisha majeruhi au wahitaji wa huduma za dharura kwa haraka, huku jingine likiwa mahsusi kwa ajili ya shughuli za uokoaji majanga kama vile moto, mafuriko na ajali.
Amesema Gari la tatu, ni kwa ajili ya Afisa Oparesheni wa Mkoa, ili kumuwezesha kufika kwa haraka katika maeneo ya dharura na kuratibu shughuli za uokoaji kwa ufanisi zaidi.
Kamanda Ngonyani amebainisha kuwa ujio wa magari hayo unatarajiwa kuongeza ufanisi wa jeshi hilo katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza mkoani humo, ikiwemo ongezeko la matukio ya ajali na majanga ya moto.
Aidha, aliwahimiza wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, huku akisisitiza kuwa usalama wa jamii ni jukumu la kila mmoja na unahitaji mshikamano wa pamoja katika kuzuia na kukabiliana na majanga.
Kwa upande wake Mkuu Wa Mkoa huo Bi, Hajjat Fatma Mwassa ametoa pongezi Kwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan Kwa kujali na kuona kuwa Mkoa huo unauhitaji Wa magari Kwa ajili ya uokozi Kwa Wananchi na kusema kuwa ni vema magari hayo yakitunzwa vizuri ili yaweze kutoa Huduma Kwa Muda mrefu.
0 Comments