Header Ads Widget

JESHI LA POLISI LATOA TAHADHARI DHIDI YA TAARIFA ZA UONGO,UCHOCHEZI LAHIMIZA AMANI KUELEKEA UCHAGUZI MKUU

 

Dodoma

Jeshi la Polisi nchini limesema hali ya usalama inaendelea kuwa shwari kote nchini kuelekea siku ya kupiga kura hapo kesho, Oktoba 29, 2025, na kwamba hakuna tishio lolote la kiusalama lililobainika hadi sasa. 

Msemaji wa Jeshi la Polisi Makao Makuu Dodoma DCP David Misime amesema jeshi limejipanga kikamilifu kuhakikisha wananchi wote wanatekeleza haki yao ya kupiga kura katika mazingira ya amani, utulivu na usalama wa kutosha.

Ameeleza kuwa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi, kumekuwa na juhudi za baadhi ya watu wachache wanaojaribu kuvuruga amani kwa njia za kidijitali baada ya kushindwa kufanya hivyo kwa vitendo, jambo ambalo jeshi limeanza kulifuatilia kwa karibu.

“Baada ya kuona wameshindwa kuvuruga amani ya nchi, watu hao wameunda kikundi cha vijana wanaotengeneza picha, video na taarifa mbalimbali bandia kuhusu matukio yanayodaiwa kutokea nchini, kisha kuzisambaza kwenye mitandao ya kijamii ili kuonesha kana kwamba ni halisi,” amesema msemaji huyo.

Aidha, Jeshi la Polisi limebainisha kuwa baadhi ya watu hao wamekuwa wakikusanya matukio yaliyowahi kutokea katika nchi nyingine na kuyawekea sauti zenye lafudhi ya Kiswahili ili kuonekana kana kwamba ni matukio ya ndani ya Tanzania, kwa lengo la kuleta taharuki na kupandikiza hofu kwa wananchi.

Vilevile, taarifa hiyo imeeleza kuwa wapo watu waliopangwa kutoa taarifa zenye maneno ya uchochezi na tungo tata zinazolenga kuchafua taswira ya taifa, huku wengine wakipanga kuchukua picha za viongozi mbalimbali na kuziwekea maneno au sauti za upotoshaji, zikionekana kana kwamba viongozi hao ndio wameyasema.

“Tunapenda kuwatahadharisha wananchi kuwa taarifa hizo ni za uongo, uzushi na zenye nia ovu ya kuchonganisha, kugombanisha na kuvuruga amani ya nchi. Wananchi wanapaswa kuwa makini na taarifa wanazoziona au kutumiwa mitandaoni,” amesema msemaji wa Polisi

Jeshi la Polisi limeongeza kuwa linaendelea kuwafuatilia na kuwakamata wote wanaojihusisha na vitendo hivyo kwa mujibu wa sheria, likiwataka wananchi wasishiriki kusambaza taarifa hizo kwani ni kosa la jinai chini ya Sheria ya Makosa ya Mtandao.

 “Iwapo utatumiwa au utaona picha, video, vipeperushi au taarifa zenye mashaka, usivisambaze. Vipuuze na uvifute mara moja. Taarifa sahihi kuhusu masuala ya kiusalama au uchaguzi hutolewa na mamlaka husika pekee,” ameongeza msemaji huyo.

Aidha Jeshi hilo l a Polisi  limewahakikishia Watanzania wote kuwa liko imara, makini na tayari kuhakikisha uchaguzi wa kesho unafanyika kwa amani na usalama katika maeneo yote nchini.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI