Header Ads Widget

IFAHAMU MIKATABA ILIYOMUWEKA RAILA ODINGA 'MADARAKANI' LICHA YA KUUKOSA URAIS.


 Jana Jumatano tarehe 15,ilikuwa asubuhi tulivu huko Kerala, India - hadi habari zilipoibuka: Raila Amolo Odinga, kiongozi wa upinzani wa Kenya na Waziri Mkuu wa zamani, ameaga dunia kwa mshtuko wa moyo wakati wa matembezi ya asubuhi. Alikuwa na umri wa miaka 80. Tangazo hilo lilileta tetemeko katika nyanja ya kisiasa ya Kenya, na kusababisha wimbi la huzuni na kutafakari katika bara zima.

Kifo cha Odinga sio tu kifo cha kiongozi wa kitaifa. Ni mwisho wa enzi ya kisiasa - inayohusishwa na harakati za upinzani, mageuzi, na nia ya kutaka kuwa rais lakini ndoto ambayo ilimponyoka kila mara licha ya yeye kuwania kiti hicho mara tano.

TAALUMA ILIYOJENGWA JUU YA MIKATABA YA KISIASA

Katika maisha yake yote, Raila Odinga alianzisha ushirikiano wa kimkakati na marais wanne wa Kenya - Daniel arap Moi, Mwai Kibaki, Uhuru Kenyatta na William Ruto. Kila mkataba ulitokana na hitaji la kisiasa, na kila moja iliacha alama ya kudumu katika utawala wa Kenya.

MKATABA NA MOI (1998–2002): KUTOKA UPINZANI HADI BARAZA LA MAWAZIRI

Baada ya kumaliza wa tatu katika uchaguzi wa urais wa 1997, Raila alishangaza taifa kwa kuingia Mkataba wa Maelewano na Rais Daniel arap Moi, mtu ambaye hapo awali alikuwa amemzuilia kwa takriban miaka tisa kufuatia jaribio la mapinduzi ya 1982. Raila alikivunja chama chake cha National Development Party (NDP) na kukiunganisha na chama tawala cha Moi cha KANU. Kwa upande wake, aliteuliwa kuwa Waziri wa Nishati mwaka wa 2001 na baadaye akawa Katibu Mkuu wa KANU.

Muungano huo ulikuwa wa muda mfupi. Mnamo 2002, Moi alimuacha Raila na kumuidhinisha Uhuru Kenyatta kama mrithi wake. Akihisi kusalitiwa, Raila aliongoza viongozi wengine kuondoka KANU, akaungana na Mwai Kibaki wa chama cha Democratic Party, na kusaidia kuunda Muungano wa National Rainbow Coalition (NARC) - muungano uliomaliza utawala wa miaka 40 wa KANU kwa kushinda uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2002.

MKATABA NA KIBAKI (2008–2013): MZOZO ULIOZAA UGAVI WA MADARAKA

Hatua ya karibu zaidi ya Raila kuchukua urais ilikuja mwaka wa 2007, alipowania urais chini ya chama cha Orange Democratic Movement (ODM). Matokeo ya awali yalionyesha anaongoza, lakini Tume ya Uchaguzi ilimtangaza Kibaki kuwa mshindi. Matokeo hayo yaliyobishaniwa yalizua ghasia za baada ya uchaguzi ambazo zilisababisha vifo vya zaidi ya watu 1,200 na wengine zaidi ya 600,000 kuwa wakimbizi.

Upatanishi wa mwezi mzima ulioongozwa na aliyekuwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan ulisababisha makubaliano ya kugawana madaraka. Raila aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu, hali ambayo ilichangia kuleta utulivu nchini. Serikali ya mseto ilidumu hadi 2013 na ilisimamia mageuzi muhimu, ikiwa ni pamoja na kupitishwa kwa Katiba ya 2010, ambayo ilianzisha ugatuzi na kupunguza mamlaka ya rais.

'HANDSHAKE' YA UHURU KENYATTA (2018): UMOJA AU KUSALIMU AMRI?


Baada ya kususia uchaguzi wa marudio wa 2017 na kujiapisha kama "Rais wa Watu," Raila alishangaza taifa kwa kupeana mkono na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Machi 9, 2018. Kusalimiana kwa mikono au 'Handshake' kulimaliza machafuko ya miezi kadhaa na kupelekea Mpango wa Building Bridges Initiative (BBI), ajenda ya mageuzi ya katiba iliyolenga kushughulikia dosari za kihistoria na kukabiliana na ukosefu wa haki.

Ingawa Raila alikanusha kunufaika binafsi, wengi wa wafuasi wake walihisi makubaliano hayo yalipunguza sauti ya upinzani. BBI baadaye ilifutiliwa mbali na mahakama, na azma ya Raila ya urais 2022 - akiungwa mkono na Kenyatta - ilimalizika kwa kushindwa na William Ruto.

MKATABA NA RUTO (2025): USHIRIKIANO BADALA YA MAKABILIANO


Mnamo Machi 2025, Raila aliingia katika Mkataba wa Maelewano na Rais William Ruto, kuashiria makubaliano yake ya nne makubwa ya kisiasa na rais aliyeko madarakani. Mkataba huo ulifuatia maandamano yaliyoongozwa na vijana na kutaka mazungumzo ya kitaifa. Yakifanikishwa kwa usaidizi kutoka kwa Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo, makubaliano hayo yalilenga kutekeleza ripoti ya Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo (NADCO).

Makubaliano hayo yaliainisha maeneo kumi muhimu ya ushirikiano, ikiwa ni pamoja na mipango ya ajira kwa vijana, kuimarisha ugatuzi, ukaguzi wa deni la taifa, ulinzi wa uhuru wa raia, mageuzi ya kupambana na rushwa, na ushirikishwaji katika utawala. Ingawa Raila alisisitiza kuwa haikuwa "kupeana mkono," ushirikiano huo uliwafanya wanachama wa ODM kuteuliwa katika baraza la mawaziri na nafasi nyingine muhimu ya serikali, na jukumu la jadi la upinzani likafifia tena.

KUGOMBEA URAIS MARA 5-BILA USHINDI

Raila Odinga amekuwa kigogo katika siasa za Kenya kwa miaka mingi

Raila Odinga aliwania urais mara tano - 1997, 2007, 2013, 2017, na 2022 - na kila mara, alikosa kupata ushindi. Kampeni zake zilishuhudia mikutano iliyohudhuriwa na watu wengi, changamoto za kisheria, na madai ya udanganyifu katika uchaguzi. Jaribio lake lenye utata na la karibu zaidi na ushindi wa kiti cha urais lilikuja mwaka wa 2007, wakati matokeo ya mapema yalipoonyesha kuwa anaongoza dhidi ya Mwai Kibaki. Lakini Kibaki alipotangazwa mshindi kwa haraka, Odinga na wafuasi wake walilalamika, na kusababisha machafuko nchini kote.

Mnamo 2022, wakiungwa mkono na Uhuru Kenyatta na muungano wa Azimio la Umoja, wafuasi wa Raila waliamini kuwa urais unaweza kufikiwa. Lakini alishindwa na William Ruto, ambaye alipata 50.49% ya kura dhidi ya 48.85% ya Raila. Mahakama ya Juu iliidhinisha matokeo hayo, na Raila akakubali, ingawa alishikilia kwamba uchaguzi huo ulikuwa na dosari.

URITHI WA UANAMAGEUZI


Safari ya kisiasa ya Odinga ilianza katika kivuli cha babake, Jaramogi Oginga Odinga, Makamu wa kwanza wa Rais wa Kenya. Lakini Raila alijitengenezea njia yake mwenyewe - kustahimili kipindi akiwa kizuizini bila kufunguliwa mashtaka, kunusurika usaliti wa kisiasa, na vuguvugu alililoongoza ambalo lilirekebisha hali ya kidemokrasia ya Kenya.

Alikuwa sogora aliyefahamu kujitunga upya kisiasa: kutoka kwa kiongozi mkali wa upinzani hadi Waziri Mkuu, kutoka kwa "Rais wa Watu" hadi mwanadiplomasia wa bara. Kampeni zake zilijaa mbwembwe, ishara, na ahadi ya kuwaongoza Wakenya hadi "Kanani" - sitiari ya kumanisha haki na ustawi.

NINI SASA KITAFUATA KATIKA SIASA ZA KENYA?


Rais wa Kenya Ruto alitoa rambirambi zake kwa mjane wa Odinga, Ida

Kifo cha Odinga kinaacha ombwe katika upinzani nchini Kenya. Muungano wa Azimio la Umoja unakabiliwa na mzozo wa utambulisho, na nchi inapania kushuhudia mirengo mipya ya kisiasa kabla ya uchaguzi wa 2027. Kutokuwepo kwake kunaweza kuwatia moyo viongozi wachanga au kuzidisha mifarakano ndani ya upinzani.

Lakini jambo moja ni hakika: Urithi wa Raila Odinga utadumu. Huenda hajawahi kukikalia kiti cha urais, lakini alibeba matumaini ya mamilioni - na kwa kufanya hivyo, alichangia kuunda mwenge wa kitaifa utakaozidi kutoa mwangaza au kuzima.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI