Na Lilian Kasenene, Morogoro
Matukio DaimaApp
CHUO Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (Higher Education for Economic Transformation(HEET), kimeanzisha utafiti maalum wa kufuatilia wahitimu wake wa miaka mitatu iliyopita (2021–2023), ili kubaini walipo, na shughuli wanazofanya.
Akizungumza katika semina ya kuwajengea uwezo watafiti kutoka SUA watakaokusanya taarifa hizo, Naibu Mratibu wa Mradi wa HEET-SUA, Dk Winfred Mbungu, alisema utafiti huo ni hatua muhimu katika kutathmini matokeo ya mitaala ya chuo na mchango wake katika kutoa elimu bora yenye tija kwa jamii.
Dk Mbungu alisema mbali na kubaini walipo watafiti hao pia wataangalia namna elimu waliyoipata imewawezeshaje kuajiriwa au kujiajiri.
“Tunataka kujua kama wahitimu wetu wameajiriwa, wamejiajiri, au wanaendelea na masomo. Taarifa hizi zitatusaidia kupanga mikakati madhubuti ya kuboresha ubora wa elimu na kuimarisha uhusiano kati ya mitaala yetu na mahitaji ya soko la ajira,” alisema Dk Mbungu.
Aliongeza kuwa ukusanyaji wa taarifa utafanyika kwa njia ya mtandao ili kupata takwimu sahihi na kurahisisha mipango ya maendeleo ya baadaye kulingana na hali halisi ya uajiri wa wahitimu.
0 Comments