Shemsa Mussa -Matukio Daima Muleba, Kagera.
Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewasili katika Mkoa wa Kagera na kuzungumza na wananchi wa Wilaya ya Muleba, ambako ameahidi kuendeleza mageuzi katika sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja na kilimo, uvuvi, mifugo, elimu, afya, na miundombinu.
Akihutubia maelfu ya wakazi wa Muleba Katika uwanja Wa zimbihile, Dkt. Samia amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali imewezesha kilimo kwa vijana 300 waliopatiwa ekari 300 kwa ajili ya kilimo cha kahawa, na wamekuwa wakizalisha miche bora pamoja na kununua trekta kwa ajili ya kuongeza uzalishaji. Ameongeza kuwa serikali inaendelea kuwekeza katika kuanzisha masoko ya wakulima ili kuwainua kiuchumi.
Kuhusu mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga, Dkt. Samia amesema mradi huo utakuwa fursa ya ajira kwa vijana wa Muleba na maeneo mengine ya mkoa wa Kagera. Ameeleza kuwa serikali itaendelea pia kuimarisha sekta za elimu na afya kwa kujenga na kuboresha miundombinu ya shule na vituo vya afya.
Katika kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa mkoa huo, Dkt. Samia amesema ni muhimu kulitumia Ziwa Viktoria kama chanzo kikuu cha maji. Ameahidi kuwa serikali itawekeza kwenye miradi ya kusambaza maji kutoka ziwani ili kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa huduma hiyo ya msingi.
Aidha, mgombea huyo amezungumzia suala la usafiri wa majini hususan katika kata za Goziba na Bumbile, ambako serikali italeta boti mbili kwa ajili ya kuboresha usafiri na shughuli za kijamii na kiuchumi. Katika sekta ya uvuvi, ameahidi kuboresha ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba, hatua itakayochochea pato la kaya na ajira kwa vijana.
Akihitimisha mkutano huo wa kampeni, Dkt. Samia amewakabidhi wagombea ubunge na udiwani nakala za ilani ya CCM, na kuwataka wananchi wa Muleba kuendelea kuiamini CCM kwa kuwapa kura za ndiyo wagombea wake wote katika uchaguzi mkuu ujao.
0 Comments