Header Ads Widget

DKT.MWINYI ZANZIBAR IMEFANIKIWA KUONDOA UBAGUZI,MIFARAKANO NA SIASA ZA CHUKI

 


Mgombea wa nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi, ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa Serikali imefanikiwa kwa kiwango kikubwa kuondoa ubaguzi, mifarakano na siasa za chuki katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Ameeleza kuwa umoja wa Wazanzibari ndio nguzo kuu ya mafanikio ya Serikali na maendeleo ya Taifa, na siyo asili ya mtu katika utoaji wa nafasi na majukumu ya kitaifa


Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali chini ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imefanikiwa kuondoa ubaguzi na kuleta maridhiano pamoja na umoja wa kitaifa kwa maslahi ya wananchi wote.

Dkt. Mwinyi ameyasema hayo alipokutana na viongozi wa dini, masheikh, watawa (masista) na mapadri katika muendelezo wa kampeni zake na utaratibu wa kukutana na makundi mbalimbali, katika ukumbi wa mikutano wa Skuli ya Utaani, Wete. Mkoa wa Kaskazini Pemba, leo tarehe 05 Oktoba 2025.

Amefahamisha kuwa mafanikio makubwa yamepatikana katika sekta za elimu, afya, ustawi wa jamii, huduma ya maji na miundombinu, na kwamba Serikali tayari imeifungua Pemba kimaendeleo na kiuchumi.

Ameeleza kuwa ujenzi wa barabara, bandari na viwanja vya ndege ni nyenzo muhimu za kuifungua nchi kiuchumi ambazo Serikali itaendelea kuimarisha katika awamu ijayo.

Rais Dkt. Mwinyi amewahakikishia viongozi wa dini na wananchi kuwa Serikali itaendelea kuyashirikisha madhehebu na dini zote bila ubaguzi katika kujadili masuala ya kitaifa na ustawi wa jamii.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Muhammed Said Dimwa, amemuelezea Rais Dkt. Mwinyi kuwa kiongozi muadilifu, mpenda amani na maendeleo, na kuwaomba wananchi wa Pemba kumchagua tena ili aendelee kuleta maendeleo zaidi.

Naye, Katibu Mtendaji wa Afisi ya Mufti wa Zanzibar, Sheikh Khalid Ali Mfaume, amesema uadilifu, haki, mshikamano na amani ni ajenda kuu za dini zinazopaswa kuzingatiwa na kila mmoja kwa ajili ya manufaa ya jamii na Taifa kwa ujumla.

Rais Dkt. Mwinyi amesema maovu yanayoendelea ndani ya jamii yanahitaji ushirikiano baina ya Serikali na taasisi za dini na kijamii kuyadhibiti, kwani si jukumu la Serikali peke yake.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ametumia fursa hiyo kuwaomba wananchi wa Pemba kumuamini kwa awamu nyingine na kumchagua tena ili aendelee kuiongoza Zanzibar kwa mafanikio na maendeleo zaidi.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI