NA CHAUSIKU SAID
MATUKIO DAIMA MEDIA ,MWANZA.
Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema serikali inaendelea kufanya tathmini ya kuvifufua viwanda vya jeneli ikiwemo cha Sengerema, Buchosa na Mwanangwa wilayani Misungwi, sambamba na kukifufua chama kikuu cha ushirika cha Vyanza ili kiweze kusimama imara na kuchochea uchumi wa wakulima wa zao la pamba.
Hayo ameyabainisha leo oktoba 8 Jijini Mwanza kampeni na kueleza kuwa hatua hiyo inalenga kuhakikisha viwanda hivyo vinazalisha nyuzi zitakazotumika kutengeneza bidhaa mbalimbali ikiwemo mashuka na bandeji zinazotumika hospitalini ili kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi.
Dkt. Samia amesema Tanzania imekuwa ikiagiza bidhaa nyingi za afya kutoka nje, ikiwemo bandeji na mashuka, wakati malighafi ya bidhaa hizo inapatikana ndani ya nchi kupitia zao la pamba linalolimwa kwa wingi katika kanda ya ziwa.
Amesema pia serikali imeanza kufufua viwanda hivyo ili viweze kuchakata pamba na kuzalisha bidhaa zinazoongeza thamani ya zao hilo, ambapo baadhi ya viwanda vitakuwa jijini Mwanza na vingine vitajengwa Itilima mkoani Simiyu.
Aidha, amesema serikali imeanza kusambaza bure mbegu na dawa za pamba kwa wakulima wa kanda ya ziwa na kuajiri vijana 700 wa huduma za ugani kwa kushirikiana na sekta binafsi ili kuboresha huduma za kilimo na kuongeza uzalishaji.
Dkt. Samia amesema kati ya matrekta 700 yaliyoagizwa, matrekta 350 tayari yamewasili nchini na yatatumika kulima kwa nusu bei, walizokuwa wakilipa kutoka sekta binafsi yakitolewa kwa vituo vya dhana za kilimo vitakavyojengwa nchi nzima, ambapo mkoa wa Mwanza utakuwa miongoni mwa Mikoa itakayonufaika.
Ameongeza kuwa serikali inaendelea na ujenzi wa uwanja wa ndege wa Mwanza utakaokuwa wa kimataifa, ambao ukikamilika utarahisisha usafiri wa watalii kuelekea Hifadhi ya Serengeti na kuchochea ukuaji wa sekta ya utalii nchini.
0 Comments