Na Ashrack Miraji Matukio Daima App
Katibu Tawala wa Wilaya ya Same (DAS), ameongoza uzinduzi wa Wiki ya Huduma kwa Wateja katika benki ya NMB tawi la Same, ambapo alitoa wito kwa wananchi kuendelea kutumia huduma mbalimbali za kifedha zinazotolewa na benki hiyo, ikiwemo kujiwekea akiba, kuchukua mikopo na kutumia huduma nyingine zinazoboresha maisha ya wananchi wa makundi yote.
Katika maadhimisho hayo, DAS alipata nafasi ya kuzungumza na wawakilishi wa wateja kutoka makundi mbalimbali katika jamii, akiwahimiza kutambua umuhimu wa huduma za kifedha katika kuleta maendeleo ya kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla. Alisisitiza kuwa Benki ya NMB imeendelea kuwa mshirika muhimu katika safari ya maendeleo ya Wilaya ya Same.
Kaulimbiu ya wiki ya huduma kwa wateja mwaka huu ni "Dhamira Inayowezekana (Mission Possible)", kaulimbiu ambayo inasisitiza uwezo wa benki hiyo katika kutimiza malengo ya kifedha ya wateja wake. Tawi la NMB Same limeitumia wiki hii kama fursa ya kutambua na kushukuru mchango wa wateja wake kwa mafanikio ya benki hiyo.
Katika hatua ya kuthamini mchango wa wateja na wafanyakazi wake, DAS alishiriki pia kugawa vyeti vya shukrani kwa baadhi ya wafanyakazi na wateja wa benki hiyo, kama ishara ya kutambua mchango wao mkubwa katika utoaji wa huduma bora kwa jamii ndani ya Wilaya ya Same.
"Ni muhimu kwa wananchi kujifunza kutumia huduma rasmi za kifedha kama njia ya kujikomboa kiuchumi. Huduma za benki ya NMB zinaweza kuwa daraja la maendeleo endapo zitatumiwa kwa weledi na malengo sahihi," alisema DAS wakati wa hafla hiyo ya maadhimisho.
Wateja waliowakilisha vikundi mbalimbali vya wafanyabiashara, wakulima, wafanyakazi wa serikali, wajasiriamali na vijana walishiriki kwa furaha maadhimisho hayo, huku wakitoa ushuhuda wa namna huduma za benki hiyo zimekuwa msaada mkubwa kwao.
Meneja wa Benki ya NMB tawi la Same, Saad Masawila, alisema wiki ya huduma kwa wateja ni wakati mahsusi wa kusikiliza, kuthamini na kuwapongeza wateja kwa uaminifu wao kwa benki hiyo. Alieleza kuwa mafanikio ya NMB hayawezi kutenganishwa na wateja wake walioweka imani katika huduma wanazozipata kila siku.
“Tunayo furaha kubwa kusherehekea wiki hii na wateja wetu ambao ndio msingi wa mafanikio yetu. Tumejipanga kuhakikisha tunaendelea kutoa huduma bora, zenye ubunifu na zinazokidhi mahitaji ya makundi yote ya jamii,” alisema Masawila.
Aliongeza kuwa benki ya NMB itaendelea kuwa mshirika wa karibu kwa wateja wake katika nyanja za kilimo, biashara ndogondogo na sekta nyingine za kiuchumi, akisisitiza kuwa huduma bora kwa mteja ndio kipaumbele kikuu cha benki hiyo katika kuhakikisha ustawi wa wananchi wa Wilaya ya Same.
0 Comments