Askofu Jacob William Kaemela wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Nyanda za Juu kusini mwa Tanzania, ametoa wito wa matumizi sahihi ya mitandao ya Kijamii na kujiepusha na uhalifu wa kimitandao pamoja na uvunjifu wa amani na sheria zilizopo nchini Tanzania.
Askofu Kaemelea ametoa rai hiyo wakati akizungumza na waandishi wa Habari Jijiji Dar Es Salaam, pembezoni mwa Kongamano la Viongozi wa Dini waliokutana Dar Es Salaam kujadili kuhusu amani kuelekea uchaguzi Mkuu wa Tanzania, akihimiza pia kujiridhisha na kila habari inayochapishwa kwenye mitandao ya Kijamii ili kujitenga na habari za upotoshaji zinazoweza kumuwema mtu matatani kulingana na sheria na miongozo ya Mitandao hiyo.
"Watu wana chaguo, unaweza kuchagua kuwa mtu mwema ukatumia vizuri mitandao ya kijamii lakini ujue tu kuwa ukitumia mitandao ya kijamii kwa nia ovu wewe utakuwa muhalifu kama muhalifu mwingine yoyote yule. Muhimu tuhimize amani, kuacha uhalifu na mitandao isitumike kama sehemu ya kufanya uhalifu." Amesisitiza Askofu Kaemela.
Akizungumzia faida ya Uwepo wa Mitandao ya Kijamii, Kiongozi huyo wa dini amebainisha kuwa imesaidia sana katika kupashana habari na taarifa mbalimbali, zaidi katika kueneza injili kwa jamii, akibainisha kuwa kwa wale wanaoitumia vibaya ni muhimu kutambua kuwa teknolojia haiondoi uhalisia wa uvunjifu wa sheria za Nchi pale mitandao hiyo itakapotumika vibaya kwa nia ya kufanya uhalifu na kutaka kuvuruga amani ya Tanzania.





0 Comments