Header Ads Widget

TUPENDANE KWA KUMAANISHA ,TUSIIGIZE -RC MWASSA AWATAKA WAISLAM KUDUMISHA UPENDO.


Na Shemsa Mussa – Matukio Daima, 

                          Kagera

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mheshimiwa Hajjat Fatma Mwassa, ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo—hasa waumini wa dini ya Kiislamu—kupendana kwa dhati, kwa kumaanisha na si kwa kuigiza, ili kudumisha mshikamano wa kidini na kijamii.

Akizungumza katika Uwanja wa Mashujaa (Mayunga) mjini Bukoba wakati wa maadhimisho ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W), RC Mwassa alikemea vitendo vya unafiki, chuki, na mafarakano miongoni mwa waumini, akisema kuwa vinaashiria upungufu wa imani ya kweli.

 "Nyie ni ndugu zangu katika Imani. Huwa nashangaa sana mtu anakuchukia na kukutukana bila sababu, na nikichunguza unakuta ni Mwislamu kama mimi. Hapo ndipo najiuliza, uko wapi undugu? Iko wapi Imani?" alisema Hajjat Mwassa.

Aliwataka Waislamu waendelee kuiga maisha ya Mtume kwa kusaidiana, kuhurumiana, na kuishi kwa amani. Aliongeza kuwa ni muhimu kwa kila mmoja kuwa na moyo wa kusamehe, kushirikiana, na kuliombea taifa kwa nia njema hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.

Aidha, RC Mwassa aliwahimiza wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao wanapata elimu ya dini kwa kuwapeleka madrasa ili waweze kujengeka kiroho na kuwa na maadili mema, jambo litakalosaidia kujenga jamii yenye mshikamano na hofu ya Mungu.

 "Kupitia madrasa tunajenga kizazi chenye uwezo wa kuitetea dini yao na kuwa na vijana wenye maadili bora katika jamii," aliongeza Mkuu huyo wa Mkoa.

Kwa upande wake, Sheikh wa Mkoa wa Kagera,  Ndg Haruna Kichwabuta, alimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa ushirikiano anaouonyesha katika masuala ya kidini, na kuwasihi waumini kujitoa kutoa sadaka ili kufungua milango ya neema na kupata radhi za Mwenyezi Mungu.

Sheikh Kichwabuta pia alisisitiza umuhimu wa watoto kusoma madrasa kwa ajili ya kuimarisha nidhamu, kufahamu sheria za dini, mavazi sahihi, na masuala ya ndoa, akieleza kuwa kutofahamu mambo hayo kunachangia migogoro mingi ya kifamilia ikiwemo madai ya talaka ya mara kwa mara.

Katika hitimisho la hafla hiyo, Masheikh na Maimam waliombwa kuendelea kusoma dua na visomo mbalimbali kwa ajili ya kulieombea taifa amani na utulivu kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.

Baadhi ya washiriki wa maadhimisho hayo walielezea furaha yao kushiriki tukio hilo, wakisema kuwa lilikuwa la kipekee na waliweza kuhisi kama wako katika mji mtukufu wa Makka kutokana na hali ya kiroho na mshikamano uliokuwepo.

Ikumbukwe kuwa maadhimisho ya kitaifa ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W) yalifanyika mapema tarehe 4 Septemba katika Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga. 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI