Na Shemsa Mussa,-Matukio Daima Media
Kagera,Chama cha Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA) kupitia kikao chake cha Kanda ya Ziwa Magharibi kimekutana na kujadili changamoto mbalimbali zinazokwamisha utekelezaji wa majukumu ya kielimu katika mikoa ya Kagera na Kigoma.
Kikao hicho kilichoandaliwa kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kuimarisha usimamizi wa taaluma mashuleni, kimeongozwa na Mwenyekiti wa TAHOSSA kanda hiyo, Dickson Mwombeki, ambaye alieleza kuwa bado kuna changamoto nyingi zinazowakabili walimu na wakuu wa shule katika Shule nyingi za Mikoa hiyo.
Akizungumza kwenye kikao hicho, Mwombeki alitaja ukosefu wa warsha na mafunzo kazini kuwa ni miongoni mwa matatizo makubwa yanayochangia kushuka kwa ubora wa ufundishaji.
“Walimu wanahitaji mafunzo endelevu ili kuwa sambamba na mabadiliko ya mitaala na mbinu za kisasa za ufundishaji,” alisema.
Ametaja Changamoto nyingine kuwa ni upungufu mkubwa wa walimu wa masomo ya lugha pamoja na msongamano wa wanafunzi unaosababisha uhaba wa samani kama meza na viti, hali inayochangia kushuka kwa viwango vya ujifunzaji darasani.
Aidha, ilielezwa kuwa utekelezaji wa mpango wa chakula mashuleni bado unakumbwa na ugumu kutokana na ukosefu wa mwongozo wa wazi kutoka kwa mamlaka husika, hali inayowapa walimu na wakuu wa shule ugumu wa utekelezaji wake.
Pia alieleza kuwepo na baadhi ya wakuu wa shule kutochangia mikutano ya kitaaluma, jambo linalowanyima fursa ya kujijenga kitaaluma na kushiriki kwenye maamuzi muhimu ya maendeleo ya elimu.
Kwa upande wake, Mgeni Rasmi wa kikao hicho ambaye ni Afisa Elimu wa Mkoa wa Kagera, Michael Ligola, alisisitiza kuwa usimamizi wa taaluma ni jukumu la kila mkuu wa shule na sio la serikali pekee.
“Matokeo mazuri ya wanafunzi hayawezi kupatikana bila usimamizi thabiti wa taaluma katika ngazi ya shule,” alieleza.
Kuhusu maandalizi ya UMISSETA, kikao kilihimiza shule kuanza maandalizi mapema ikiwemo ukusanyaji wa fedha kuanzia ngazi ya shule hadi halmashauri pamoja na kuanzisha vitaru vya michezo ili kukuza vipaji vya wanafunzi na kubadili mitazamo kuhusu umuhimu wa michezo.
Katika hatua nyingine, viongozi hao walikubaliana kuwa wanafunzi wa kidato cha pili na cha nne wanapaswa kuwepo kambini karibu na shule kabla ya mitihani yao, ili kujenga utulivu wa kimasomo na kuboresha ufaulu.
MWISHO.
0 Comments